Naibu Waziri wa Madini,Dkt Steven Kiruswa na Mbunge wa Jimbo la Longido Mkoani Arusha amewataka Watendaji wote ngazi ya Kitongoji ,Kijiji ,Kata na Wilaya kuhakikisha wanafuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi yote ya Maendeleoa katika wilaya ya Longido Mkoani Arusha ili Serikali iweze kuiamini wilaya hiyo na kuendelea kupeleka fedha za Miradi.

Dkt Kiruswa alisema hayo jana wakati akiwa mgeni rasmi katika Harambee ya Ujenzi wa ofisini ya Chama Cha Mapinduzi{CCM} Wilaya ya Longido ambapo awamu ya kwanza zilihitahika shilingi milioni 49  lakini katika harambee hiyo makusanyo yalivuka malengo na kufanikiwa kukusanya shilingi milioni 40.5 fedha taslimu na shilingili milioni 31.5 ahadi na kufanya Harambee hiyo kukusanya jumla ya shilingi milioni 72.

Harambee hiyo ilihudhuriwa na Madiwani wote wa Halmashauri ya Longido,Watendaji wa vijiji ngazi ya kijiji na kata,viongozi wa CCM ngazi zote na viongozi wa Jumuiya zote za chama.

Alisema Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inajali wananchi wa Wilaya ya Longido na ndio maana inapeleka fedha nyingi katika miradi ya elimu ,afya ,maji na barabara hivyo watendaji wote wa ngazi zote wanapaswa kuwajibika kila mmoaja kuhakikisha miradi hiyo inakamilika katika muda muafaka ili Rais aendelee kuwaamini na kupeleka fedha zaidi katika wilaya hiyo.

‘’Nawaomba viongozi wenzangu kwa pamoja tuhakikishe tunasimamia miradi yote ya Maendeleo katika Wilaya ya Longido ili tuweke alama ya uongozi na sio vinginevyo’’alisema Dkt Kiruswa

Akizungumzia mradi wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa ofisi ya CCMna Jumuiya zake,Dkt Kiruswa alisema kuwa mradi huu unapaswa kukamilika kabla ya Disemba 31mwaka huu ili januari mwakani watendaji wa chama wawe ofisini.

Dkt Kiruswa alisema na kuwataka waliopewa majukumu ya kusimamia ujenzi wa mradi wa chama yaani kamati ya ujenzi kuhakikisha fedha zilizokusanywa zinatumika katika malengo yaliyokusudiwa na sio vinginevyo.

Alisewma yeye na marafiki zake wamefanikiwa kuchangia kiasi cha shilingi milioni 15 ,Madiwani ,watendaji wa kata na vijiji katika kata zote 18 wa jimbo hilo wamechangia kiasi cha shilingi milioni moja kila kata,ofisi ya CCM Wilaya imeahidi kuchangia shilingi milioni moja katika harambee hiyo.

Mbunge alisema awamu ya pili ya mradi huo utagharimu zaidi ya shilingi milioni 426 na harambee yake inatarajiwa kufanyika mapema mwakani kwani ujenzi wa ofisi za chama ni moja ya ahadi zake wakati akiomba ridhaa ya Ubunge katika Jimbo hilo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido,Saimon Oitesoi amemwakikishia Mbunge kuwa fedha zote za miradi katika wilaya hiyo ziko mikono salama na zitatumika kama zilivyokusudiwa na kwa wakati muafaka.

Oitesoi alisema kuwa hakuna fedha za mradi itakayoliwa na mtu yoyote awe mwanasiasa na mtendaji wa ngazi zote kwani Kamati ya fedha na Madiwani wote wa Halmashauri ya Longido wako macho kuhakikisha kila kitu kinatimizwa kwa maslahi ya wananchi wa Longido.

Alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ametuma fedha za miradi yote katika Jimbo la Longido hivyo wao kama wasimamizi wa miradi hawawezi kuona fedha zinaliwa na miradi haifanyi kazi wakakaa kimya hilo halipo na halitakuwepo katika Wilaya ya Longido.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Longido,Papaa Nakuta aliwataka madiwani wa chama hicho kuwa kitu kimoja kukijenga chama na kuacha mara moja makundi kwani hayana faida ndani ya chama.

Nakuta alisema wajibu wa Diwani katika kata ni kusimamia miradi yote ya maendeleo katika eneo husika na kukisemea vizuri chama kilichomweka madarakani na kuacha mara moja makundi na kuwabeza baadhi ya viongozi waliochaguliwa kwa kufanya hivyo ni kosa kikanuni kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Alisema na kuwataka madiwani kujianda na uchaguzi wa serikali za mitaa ili kila diwani awajibike kwa hilo na kila kata chama kiweze kupata ushindi wa kishindo kwani siri ya ushindi ndani ya chama ni ushirikiano na sio vinginevyo.

Share To:

ASHRACK

Post A Comment: