Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd; kampuni inayomiliki Mradi wa Umeme unaotokana na chanzo cha maji wa Ijangala (Ijangala Mini Hydro Power Project) Bwana Elikana Kitahenga, amesema leo Tarehe 4 Septemba, 2023 wanataraji kuandika historia ambapo Mradi huo utaanza rasmi mchakato wa kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa baada ya kukamilika kwa hatua ya mwisho za ujenzi wa kituo hicho.

Mradi wa Umeme unaotokana na chanzo cha maji wa Ijangala kwa sasa una uwezo wa kuzalisha KiloWati 360 ambapo kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa maana yake ni kuwa kampuni ya Nishati Lutherani (DKK) Investment Ltd itaanza kuuza umeme huo kwa Shirika la Umeme la Tanzania (TANESCO).

Akiongea na Wanahabari; Mkurugenzi Mkuu, Bwana Kitahenga amesema kukamilika kwa hatua hii ya kuanza kuingia Mradi wa Ijangala kwenye Gridi ya Taifa; kumetokana na uwezeshaji wa rasimali fedha kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo mwaka 2013, Mradi huo ulipokea awamu ya kwanza, shilingi milioni 133 na baadae mwaka 2016 Mradi ulipokea awamu ya pili, shilingi milioni 426 na awamu ya tatu, wanataraji kupokea shilingi milioni 437.

Jumla ya fedha shilingi 996 kutoka Serikalini kupitia REA zitakuwa zimewezesha kukamilika kwa Mradi huo ambao, imeelezwa kuwa utakuwa ukombozi wa Wananchi wa vijiji vya Masisiwe, Tandala, Ikonda, Usagatikwa na Ihela ambapo zaidi ya watu 4,000 watanufaika moja kwa moja kwa kupata umeme wa uhakika utatokana na Mradi wa chanzo cha maji wa Ijangala.

Akieleza kuhusu tukio la kuingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa; Mshauri Elekezi wa Mradi huo wa Ijangala Prof. Zakaria Katambala kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) amesema kazi imefanywa vizuri na Wakandarasi wanne (4) na kuongeza kuwa matarajio yake ni kuwa baada ya wiki moja zoezi la kuunganisha Kituo hicho na Gridi ya Taifa litakamilika.

Amezitaja kazi zilizofanywa na Wakandarasi hao wanne (4) kuwa ni pamoja na ujenzi wa bwawa linalokinga maji kutoka juu kuja chini ulipo Mradi (Power Hous); kazi nyengine ni ujenzi wa bomba la kusafirisha maji (Penstock) kutoka juu kuja chini kwenye mtambo wa kufua na kuzalisha umeme; kazi ya tatu ni ujenzi wa sehemu ya kuzalisha umeme (Power House) na sehemu ya mwisho ni ujenzi wa mfumo wa kuunganisha mtambo wa umeme wa chanzo cha maji ili uungane na umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

“Kazi imefanyika vizuri, na tunatarajia Wawakilishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufika hapa eneo la Mradi ili kuja kuangalia ubora wa kazi yetu na baada ya kujiridhisha, wataturuhusu kuanza kuingiza umeme unaozalishwa hapa kuingia kwenye Gridi ya Taifa”. Alisema Profesa Katambala.

Akizungumzia kuhusu zoezi hilo la kuingiza umeme unaozalishwa na Mradi wa Umeme unaotokana na chanzo cha maji wa Ijangala kuingia kwenye Gridi ya Taifa; Mkurugenzi Mkuu, Bwana Kitahenga amesema zoezi hilo linataraji kushirikisha Wataalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mkandarasi aliyejenga njia ya umeme kuja kwenye chanzo cha kuzalisha umeme cha Ijangala; kampuni ya SILO na kuongeza kuwa linataraji kuendelea kwa wiki mbili hadi tatu.





Share To:

Post A Comment: