Na; Elizabeth Paulo, Dodoma

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. David Silinde ametoa rai kwa Wafugaji nchini kuwa mifugo ni Utajiri hivyo kuongeza uzalishaji wenye tija na wa kibiashara ili kuongeza Ajira, Kipato, Kupiga vita umaskini na kuchangia uchumi wa nchi.


Mh. Silinde amesema hayo  Agost 05, 2023 Jijini Dodoma alipokua akifungua maonesho na mashindano maalum ya mifugo kitaifa katika viwanja vyangu Nzuguni.


“Kuendelea kufanyika kwa mashindano haya na mashindano haya kumechangia , kuhamasisha, Kukuza na kuendeleza ufugaji bora hapa nchini.”Amesema Silinde


Amesema Ili kuhakikisha tija inapatikana kupitia Sekta ya Mifugo, Wizara imeweka vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo, Kuimarisha afya ya mifugo, Kuboresha huduma za ugani, Kuimarisha huduma za utafiti na mafunzo ya taaluma za mifugo, Kuimarisha masoko, na kuwezesha uongezaji thamani mazao ya mifugo na uvuvi.


Naibu Waziri huyo amesema mashindano kama hayo hufanyika katika nchi mbalimbali yakiwa na lengo la kutambua mchango na juhudi za wafugaji katika kuchangia maendeleo ya Taifa na mtu mmoja mmoja.



Aidha maonesho haya huongeza ari kwa wananchi kuongeza uzalishaji na tija kwa kutumia teknolijia mpya na zilizoboreshwa kukidhi mahitaji ya soko.


“Maonesho na mashindano haya ya mifugo ambayo hadi leo hii yanafanyika kwa mara ya kumi na mbili (12) mfululizo kitaifa hapa Dodoma tangu kuasisiwa na Mhe. Jakaya Kikwete Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2010 katika siku ya kilele cha sherehe ya nanenane.”Amefafanua Silinde



Mhe. Silinde amesema Wizara inaangalia namna bora yakufanya maonesho hayo kuwa na taswira na hadhi ya Kitaifa kama ilivyokusudiwa ambapo wafugaji walioshinda katika kanda mbalimbali watakuja Dodoma kushindana Kitaifa huku akisema Wizara itaendelea kuboresha tuzo na zawadi wa washindi ili kuwapa hamasa zaidi wafugaji kuleta mifugo yao kwenye mashindano.


Awali Akitoa salamu za Mkoa Mheshimiwa Rosemary Senyamule Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amesema Kwa mujibu wa sensa ya Kilimo ya mwaka 2021, Mkoa wa Dodoma ni wa tano kwa wingi wa ng'ombe ukikadiriwa kuwa na ng'ombe zaidi ya 2, 195, 576 ukizidiwa kwa mifugo na Mikoa ya Tabora, Arusha, Simiyu, na Manyara.



Amesema Sekta ya Mifugo inao umuhimu wa peke kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma kutokana na kuwa ni chanzo cha chakula, Kipato, Nguvu kazi, Mbolea, Fahari, Zawadi na hata kwa ajili ya kufanyia malipo ya aina mbalimbali kama mahari.




Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: