Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa Tanzania wa chama cha mapinduzi UWT Taifa, Bi. Zainabu Shomar ameiasa jamii kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania SMAUJATA  katika juhudi za kupinga ukatili.

 

Ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 28,2023 wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Isaka Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama ikiwa ni sehemu ya ziara ya UWT Taifa, Mkoani Shinyanga.

 

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa kampeni ya kupinga ukatili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga ambapo pamoja na mambo mengine Bi. Zainabu Shomar ameitaka jamii kutofumbia macho vitendo vya ukatili vinavyoendelea kutokea katika jamii hasa kwa wanawake na watoto.

 

Bi. Zainabu Shomar ametumia nafasi hiyo kuwapongeza viongozi wa kampeni ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kwa utekelezaji wa majukumu yao katika kuibua masuala la ukatili huku akiwaomba wananchi kushirikiana na kampeni hiyo ili kutokomeza ukatili unaoendelea katika jamii.

 

Amewasisitiza wananchi  kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika juhudi za kulinda maadili,ambapo amehimiza wazazi na walezi kuwekeza zaidi kwenye malezi na makuzi bora kwa watoto huku  akikemea tabia inayofanywa na baadhi ya wanaume wanaofanya udhalilishaji kwa wanawake na watoto.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Bwana Solomon Nalinga Najulwa amesema kampeni hiyo itaendelea kushirikiana na UWT pamoja na viongozi wengine wa serikali katika hatua za kuibua na kupinga ukatili.

Kampeni ya SMAUJATA inafanyakazi zake chini ya Wizara ya  maendeleo ya jamii jinsia, wanawake na makundi maalum inayoongozwa na Waziri Dkt. Dorothy Gwajima ambayo ilianzishwa na Waziri huyo kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa SMAUJATA Taifa Bwana Sospeter Bulugu ikiwa lengo ni kuisaidia serikali kutokomeza ukatili Nchini.

Nao baadhi ya wanawake wa kata ya Isaka wilayani Kahama wamesema licha ya juhudi mbalimbali zinazoendelea katika kupinga ukatili lakini wameviomba vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa wanaobainika kuhusika na matukio ya ukatili.

 

Wananchi hao wa kata ya Isaka wakiwemo wanawake wameiomba serikali kutowafumbia macho wale wote wanaobanika kufanya ukatili hasa kwa wanawake na watoto ambapo wamesema mmoja ya changamoto zinazosababisha mmomonyoko wa maadili ni baadhi ya wanaume kutelekeza familia zao na kukimbia kusikojulikana.

Viongozi wa Jumuiya ya wanawake wa Tanzania  wa chama cha mapinduzi UWT Taifa wameendelea na ziara kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.

 

Katika kata ya Isaka umoja wa wanawake Tanzania  UWT umetembelea na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo Bweni la Wasichana na Bweni la Wavulana katika shule ya sekondari Isaka ambapo Mwenyekiti wa UWT kata ya Isaka Bi. Nabila Kisendi amewapongeza na kuwashukuru viongozi wa UWT kwa kutekeleza lengohilo la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa Tanzania wa chama cha mapinduzi UWT Taifa, Bi. Zainabu Shomar akizungumza kwenye mkutano huo kata ya Isaka Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga leo Jumatatu Agosti 28,2023. 

Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Mhe. Gasper Kileo akizungumza kwenye mkutano huo, kata ya Isaka Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga leo Jumatatu Agosti 28,2023. 

Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Shinyanga Santiel Kirumba akizungumza kwenye mkutano huo, kata ya Isaka Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga leo Jumatatu Agosti 28,2023. 


Mwenyekiti wa UWT kata ya Isaka ambaye pia ni Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bi. Nabila Kisendi akizungumza kwenye mkutano huo, kata ya Isaka Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga leo Jumatatu Agosti 28,2023. 

Mwenyekiti wa kamati ya maadili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Solomon Najulwa Nalinga jina maarufu Cheupe akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga leo kwenye mkutano huo, kata ya Isaka Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga leo Jumatatu Agosti 28,2023. 

Awali akiwasili Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa Tanzania wa chama cha mapinduzi UWT Taifa, Bi. Zainabu Shomar katika mkutano huo leo Jumatatu Agosti 28,2023.


Share To:

Misalaba

Post A Comment: