Imeelezwa kuwa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na wadau wengine wako mbioni kukamilisha mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya Wachimbaji Wadogo ili kuhakikisha inasaidia kundi hilo kupata mitaji kupitia mikopo na hatimaye kujikwamua kiuchumi pamoja na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika pato la taifa.

Hilo limeelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, Agosti 28, 2023, wakati akizungumza katika Mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa wazo hilo liliasisiwa kwenye Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika jijini Mwanza mwezi Mei 2023, na baadaye kuundiwa kamati kwa ajili ya kushughulikia mchakato huo jijini Arusha.

Dkt. Mwasse amesema kuwa kuwa Uanzishwaji wa benki hiyo umelenga kutatua changamoto ya ukosefu wa mitaji inayowakabili wachimbaji wadogo nchini jambo linalowasabisha washindwe kufanya uchimbaji wenye tija na kufikia malengo yao.

“Tuliingia makubaliano ya mashirikiano na taasisi nyingine za fedha kwa ajili ya kukopesha wachimbaji wadogo, lakini niseme kuwa uzoefu unaonyesha kuwa sekta hii ya madini ina sifa zake ambazo taasisi zingine zinashindwa kukubaliana na taratibu na hizi benki za kawaida” amesema Dkt Mwasse

Aidha, Dkt. Mwasse ameeleza kuwa STAMICO imeweka lengo la kuwaendeleza wachimbaji hao wadogo kwa kuwarasimisha kabisa ili wafanye shughuli zao bila usumbufu kwa kuwa wengi wao wanachimba madini ili wajipatie kipato cha kuendeleza familia zao.

Amesema katika kuhakikisha wanafikia lengo hilo, shirika litaendelea kuwapa mafunzo ambako tayari wanazunguka nchi nzima kuwafikia, kuendelea kuwajengea uwezo kwa upande wa teknolojia mpya kwa kuwaletea vifaa vya kisasa zaidi sambamba na kuanzisha benki hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile ameipongeza STAMICO kwa hatua kubwa waliyofikia katika kutimiza malengo na kuwaomba kuendelea kuvishirikisha vyombo vya habari kwa kila hatua ili wananchi waweze kujua kiundani mafanikio makubwa ya Shirika hilo la Madini la Taifa.

Share To:

Post A Comment: