Takribani watu 210 wamejitokeza kupima homa ya Ini katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ambapo 13 kati yao wameanzishiwa  matibabu baada ya kubainika kuwa na maambukizi.

Watu hao wamepata huduma hiyo kupitia kampeni maalumu ya kupima na kupata chanjo ya homa ya Ini iliyotolewa katika Hospitali hiyo, tangu Julai 26 hadi Julai 28 Mwaka huu 2023, ambapo watu 197 hawakukutwa na maambukizi lakini wameshauriwa juu ya umuhimu wa kupata chanjo ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtaalam wa idara ya magonjwa ya ndani wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga,Dkt. Emmanuel Sadiki amesema tayari wagonjwa 76 kati ya 197 ambao hawakukutwa na maambukizi, wamepata chanjo ya kujikinga na homa ya ini, kati yao wanawake ni 42  na 32 ni wanaume.

Dkt. Sadiki amezitaja baadhi ya dalili za ugonjwa wa homa ya Ini lakini pia madhara ambapo amesema husababisha kiwango kikubwa cha sumu inayochangia kuharibu mfumo wa ubongo.

“dalili za awali ni pamoja na kusikia uchovu,homa,maumivu ya kichwakchefu chefu na wakati mwingine kutapika,lakini tatizo likikomaa utaona dalili za manjano,maumivu ya tumbo juu upande wa kulia na dalili nyingine”kwa hiyo ukiona dalili hizo wahi hospitali ili uweze kupata huduma ikiwemo vipimo,alisema Dkt Sadiki

Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga imetoa huduma ya kupima na kutoa chanjo ya homa ya Ini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya homa ya Ini Duniani, ambapo zoezi hilo lilifanyika sanjari na utolewaji wa elimu, ushauri na  kutoa matibabu kwa watu wanaobainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Dkt. Emmanuel Sadiki ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa na utamaduni wa kupima homa ya Ini na magonjwa mengine ili wakibainika kuwa na maambukizi waanze matibabu mara moja na kwa wale ambao hawatakutwa na maambukizi waweze kuchukua tahadhari ya kujikinga

Kwa upande wao wananchi waliopata huduma ya kupima wameshukuru na kupongeza juhudi za serikali kupitia Wizara ya Afya kuweka utaratibu huo mzuri wa Wananchi kupata elimu sahihi juu ya huduma za afya,ushauri,kupima chanjo, na matibabu kwa wale wanaobainika kuwa na maambukizi.

Seleli Ngassa mkazi wa kijiji cha Jomu kata ya Tinde Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga,ni mmoja wa Wananchi waliopata chanjo ya kujikinga na maambukizi ya homa ya ini katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shiyanga, baada ya kupimwa na kukutwa hana maambukizi,ambapo ameeleza kutokana na kupata ushauri na elimu sahihi juu ya huduma hiyo,amechukua hatua ya kupata chanjo hiyo  ikiwa ni tahadhari ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo wa homa ya ini

“baada ya kupima majibu yalionyesha sina maambukizi,kwanza nilifurahi sana,nilitoa machozi ya furaha,na nikamwambia mtoa huduma anipatie chanjo,kwa kuwa kabla ya kupima,tayari nilikuwa nimepata ushauri na elimu,kwa hiyo nikapata chanjo hiyo ili kujikinga na maambukizi” ameeleza Ngassa.

Kulthum  Mwangia Mkazi wa kata ya Ndala katika Manispaa ya Shinyanga alisema maboresho yanayoendelea kufanywa na Wizara ya Afya katika utoaji wa huduma yanasaidia kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika.

“inasadia sana kuzuia vifo kwa watu ambao pengine wasingepata huduma ya kupima wasingebaini tatizo,hali ambayo ingechangia tatizo kukomaa mwilini na mwisho wa siku hata akifika hospitali kwa ajili ya kupata tiba,atapoteza maisha kwa kuwa atakuwa amechelewa na tatizo litakuwa kubwa”amesema Zuhura

 

MWISHO

Share To:

Misalaba

Post A Comment: