Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha wanakamilisha Ujenzi wa Shule ya Msingi Msagali ndani ya muda wa wiki mbili baada ya kutokamilika kwa muda uliopangwa awali wa tarehe 30 Juni, 2023.

Senyamule ameyasema hayo Agosti 1, 2023 wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Mpwapwa kukagua miradi na miundombinu inayojengwa katika Shule hiyo Mpya ya Msagali inayojengwa kupitia fedha za Boost na Shule ya Sekondari Mazae kupitia fedha za Serikali Kuu.

Aidha, kiasi cha ya shilingi Milioni 493 zimetolewa kupitia mradi wa boost kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya viwili vya madarasa ya mfano kwa Elimu ya awali vyeye matundu sita (6) ya vyoo, Vyumba 14 vya Madarasa, Matundu ya vyoo kumi na sita (16), Jengo la Utawala, Kichomea taka, madawati, viti na meza katika Shule ya Msingi Mpya ya Msagali. 

Pia, kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 730 zimetolewa katika Shule ya Sekondari Mazae kwa ajili ya Ujenzi wa Madarasa tisa (9), Mabweni manne (4) na Matundu ya vyoo kumi na nne (14).

"Nawapatia wiki mbili hii shule iwe imekamilika hakikisheni mnachukua hatua na kuandaa mpango kazi ambao utakamilisha kazi hii kwa haraka pia vifaa vyote vinunuliwe, hapa najua pamoja na yote mnayojitetea kuna chembe chembe ya uzembe "ameonya Senyamule 

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa huyo ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya Ujenzi wa Mabweni ya Shule ya Sekondari Mazae na kuwataka kujipanga vizuri kwa hatua zote kwani muda uliosalia wa kidato cha tano kuwasili shuleni hapo umekaribia. 

"Kwenye upande wa Madarasa niwapongeze, Ila mabweni lazima siku zilizobaki tujipange vizuri na tuhakikishe yanakamilika kwa wakati, wapo watoto watakao toka Mikoa mbalimbali watahitaji kukaa bweni hakikisheni mnayamaliza sasa zimebaki wiki mbili tuone hamlali usingizi mfanye kazi nyingi kwa wakati mmoja ili tusimwangushe Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini ambacho hakijanifurahisha zaidi mnaleta vifaa nusu nusu zingatieni maelekezo tunayotoa kama Mkoa, Mjipange vifaa ambavyo havipo hakikisheni mnavinunua "ameeleza Senyamule 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpwapwa Mhe. George Fuime ameahidi kuyasimamia kikamilifu maagizo yaliyotolewa na Mhe. Senyamule kwa kuongeza nguvu kazi na kupanga mpango Mkakati utakaowasaidia kukamisha miradi hiyo kwa wakati.

Share To:

Post A Comment: