Maafisa watendaji wa kata na vijiji wilaya ya Arumeru inayojumuisha halmashauri mbili za Arusha na Meru, wamekutana na kukumbushana utekelezaji wa majukumu yao  unaozingatia kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa Umma.

Maafisa hao wamepewa somo hilo na mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda kwa kushirikiana na Watalamu wa fani mbalimbali, wakati wa kikao kazi cha siku moja, chenye lengo la kuwajengea uwezo ili kuwa na uelewa wa pamoja juu ya usimamizi wa fedha na miradi ya maendeleo pamoja na kukumbushana utekelezaji wa majukumu yao, kikao ilichofanyika kwenye ukumbi wa shule ya  wa Fikiria Kwanza eneo la USA-River.

Mkuu huyo wa wilaya ameweka wazi kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kuwajengea uwezo na uelewa wa pamoja usimamizi na utunzaji wa fedha za Umma, kujadili changamoto zinazowakabili pamoja na  kukumbushana utekelezaji wa majukumu yao kwa serikali na wanannchi.

Aidha ameeleza kuwa, kutokana muundo na lengo la Serikali kugatua madaraka kwa Serikali za Mitaa ni kusogeza huduma karibu na wananchi, hivyo Maafisa Watendaji, wanayo dhamana kubwa ya kuwajibika katika mnyororo mzima wa agenda ya kusukuma gurudumu ka maendeleo ya jamii na Taifa kwa  kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwenye maeneo yao, kupitia ofisi za kata na vijiji.

"Mtendaji wa kata na kijiji, Serikali imekupa dhamana kubwa ya kusimamia shughuli zake zote za serikali katika eneo lako,  tambueni kuwa majukumu makubwa ya serikali za mitaa yako mikononi mwenu, nyinyi ndio wasimamizi na watekelezaji wa shughuli zote za maendeleo ya nchi hii, hakikisheni mnafanya kazi kwa waeledi kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zinazoelekezwa na serikali, tumieni hekima, busara na maarifa kutekeleza majukumu yenu". Amesisitiza Mhe. Emmanuela

Amewakumbusha majukumu yao ni usimamizi wa shuguli zote za serikali katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa fedha zote za Umma katika maeneno yao, usimamizi wa miradi ya maendeleo, ulinzi wa amani, wasimamizi wa watalamu kweny maeneo yao.

Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya amekemea tabia ya baadhi ya watedaji, kutokuwa waaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa kufanya vitendo ambavo ni kinyume na maadili ya utumishi wa Umma, wapo wanaofanya ubadhilifu wa fedha za Umma, matumizi ya fedha yasiyozingatia taratibu, na baadhi yao kuungana na wenyeviti wa vijiji na wenyeji kuuza maeneo kwa njia zisizo halali jambo linalosababisha migogoro na wananchi kukosa haki zao na baadhi kutokuwa na imani na serikali yao.

"Baadhi ya watendaji mmekuwa sio waaminifu mmesababisha migogoro na kuwaacha wananchi kuwa na kero na malalamiko mengi kwa kuwanyima haki zao kwa maslahi yenu binafsi, ninawaasa mkiwa kama viongozi wekeni mbele maslahi ya Umma, fanyeni kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi, simamieni haki na wajibu wenu ili kila mwananchi wapate haki yake, msiwe chanzo cha migogoro kwenye maeneo yenu". Amesisitiza Mhe. Emmanuela

Awali kikao kazi hicho kilichobeba mada za Majukumu ya Watendaji wa kata na vijiji, matumizi ya mifumo ya malipo na ukusanyaji wa mapato ya fedha za Umma, taratibu za utoaji wa vibali vya ujenzi, jukumu la Watendaji katika  mapambano dhidi ya rushwa, Ushiriki wa Watendaji katika kuimalisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.

Share To:

Post A Comment: