Na John Walter-Manyara

Maafisa usafirishaji abiria na mizigo (Madereva bodaboda) mkoa wa Manyara wamelipongeza jeshi la polisi kwa ushirikiano wao uliosaidia kupunguza vitendo vya uhalifu mkoani humo ikiwemo uporaji wa pikipiki.

Wakizungumza katika tamasha la Nyama Choma lililoandaliwa na jeshi hilo pamoja na Boda boda na Bajaji, Viongozi wa Boda boda John Faustin wa Hanang' na mwenyekiti wa mkoa Adam Omari, wamesema kulikuwa na changamoto ya kuibiwa pikipiki lakini tangu wameungana  na jeshi la polisi jambo hilo halipo tena kwa kuwa wanashirikiana kwa kutoa taarifa.

"Ukiweza kukaa na maafisa usafirishaji kama leo ukawafundisha polisi jamii ni nini na kazi zake na mbinu za kuwatambua wahalifu, mkoa wako wa Manyara utakuwa shwari" Adamu Omari Mwenyekiti wa Boda boda mkoa wa Manyara

Hata hivyo wamelitaka Jeshi hilo nchini kuendelea na udhibiti wa uhalifu kwani limeleta amani na kuongeza ari ya ufanyaji kazi kwa bodaboda mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara George Katabazi amewapongeza kwa kuonyesha ushirikiano wa dhati katika kutanzua, kupambana na kuzuia uhalifu huku akisema wilaya ya Hanang imekuwa mfano wa kuigwa.

Katabazi amewataka maafisa usafirishaji hao waendelee kutii sheria bila shuruti ili waendelee kubaki salama.

Naye mkuu wa usalama bara barani mkoani hapa Fredrick Mpolo amewakumbusha Madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha na kuepuka ajali.

Share To:

Post A Comment: