Na Elizabeth Joseph, Monduli.
KAMATI ya Fedha,Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Monduli imewaagiza Wataalamu wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Shule ya Awali na Msingi (Boost) kuzingatia viwango vinavyohitajika.
Maagizo hayo yametolewa na Kamati hiyo wakati ya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kata mbalimbali za Wilaya hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli Mh,Isack Kadogoo ambapo hawakuridhishwa na viwango vya milango,uwekaji wa Madirisha pamoja Vigae katika baadhi ya Shule zinahusisha mradi wa Boost.
"Wataalamu msitafute mchawi,tuache ubabaishaji na kukwamisha watu waliopo Site,mafundi wana mapungufu yao na ninyi mna mapungufu yenu,kila mmoja ana mapungufu yake hakikisheni mnasimamia na kufuatilia vizuri ujenzi wa miradi hii ili kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu ambaye ametupatia fedha hizi."
"Mheshimiwa Rais anahangaika kila siku kuhakikisha anatengeneza vyanzo vya mapato ili atuletee fedha kama hii ya Boost peke yake ni zaidi ya Bilioni 1.7 lakini sisi wana Monduli kazi ndogo tuliyopewa katika miradi hii ni kusimamia hivyo niwaombe kila mmoja atimize wajibu wake"alisema Mh, Kadogoo.
Aidha aliagiza ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kutenga fedha ya mafuta kwaajili ya Idara ya Ujenzi ili kusaidia Idara hiyo kufanya ukaguzi katika miradi inayoendelea kujengwa wilayani humo kwakuwa katika ziara hiyo ya ukaguzi mapungufu mengi yaliyooneka a yamesababishwa na kukosa ukaguzi wa mara kwa mara.
"Sasa kama serikali imetuletea mamilioni ya fedha sisi Halmashauri tunashindwa kununua Lita 1000 ambayo ni Milioni 2,857,000 tukasema hii ni kwaajili ya Ma Engineer kufanya supervision na kwenye hili nimeruhusu tumieni hata gari yangu ili kufanya kazi hii ya supervision ili kupata kazi nzuri yenye viwango na yenye kueleweka'' aliongeza kusema Mwenyekiti huyo.
Pia alipongeza baadhi ya Wakuu wa Shule na Uongozi wa Kata na Kijiji kufanya vizuri katika utekelezaji wa miradi hiyo na kuwataka kuhakikisha wanamaliza kazi zilizobaki ikiwemo ujenzi wa vyoo,kupaka rangi na uwekaji wa Madirisha.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli Bw,Ludwig Ngakoka aliiahidi kamati hiyo kuhakikisha mapungufu yote yalioonekana katika miradi hiyo yanatekelezwa kulingana na viwango ambavyo Serikali inataka vifuatwe.
Naye Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Monduli Bi,Natang'aduaki Mollel licha ya kuipongeza kamati hiyo kwa ukaguzi wa miradi pia aliwashukuru wananchi wa Kata ambazo miradi hiyo inatekelezwa kwa kujitoa kushiriki katika kufanikisha miradi hiyo inatekelezwa ikiwemo kusomba mawe na kuchimba msingi.
Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ilitembelea na kukagua miradi ya Ujenzi na Ukarabati wa vyumba vya Madarasa Shule ya Awali na Msingi,Majengo la Utawala,nyumba ya Walimu,Ujenzi wa Vyoo pamoja na Zahanati ambayo ipo katika Kata ya Monduli Juu,Moita, Makuyuni,Esilalei,Migungani na Kata ya Selela ambapo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ilitoa zaidi ya Bilioni 1 ikiwa ni fedha za Boost huku ujenzi wa Zahanati ya Ranch katika Kijiji cha Selela ukitumia Mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Boost ni mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Shule za Awali na Msingi Tanzania Bara ambayo pia ni sehemu ya mpango wa Lipa kulingana na Matokeo EP4R.
Post A Comment: