Na Elizabeth Joseph,Monduli.


ZAIDI ya Milioni 584 zinatarajiwa kujenga Shule mpya ya Sekondari katika Kata ya Lepurko iliyopo wilayani Monduli ikiwa ni lengo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika kuinua elimu nchini.

Hayo yalibainishwa na Afisa Elimu.Sekondari Wilaya ya Monduli Bi,Magreth Muro wakati wa ziara ya ukaguzi wa eneo ujenzi wa Shule hiyo iliyohusisha Kamati ya Fedha,Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Monduli pamoja baadhi ya wakuu wa Idara.

Bi Muro alieleza kuwa wamepokea fedha hizo kutoka serikalini kwaajili ya ujenzi wa Shule hiyo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni kwa kuanza na uchimbaji wa msingi ambao alisema wananchi wa Kata hiyo wameahidi kushiriki kuchimba pamoja na kukusanya nawe.

 "Awamu ya kwanza itahusisha majengo ya Utawala,Maabara 3 ya Physics, Chemistry na Biology pamoja na jengo la TEHAMA lakini pia tutakuwa na jengo la Maktaba,vyoo vya Wasichana na Wavulana na kisima cha chini cha kuwekea maji huku nyumba ya walimu itakuja kwenye awamu ya pili ya ujenzi"alifafanua Bi.Muro.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli Mh.Isack Kadogoo aliipongeza serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuisaidia Halmashauri hiyo katika sekta ya elimu kwani Shule hiyo ni ya tatu wilayani humo kupata fedha kwa asilimia 100 kutoka serikalini.

Aidha Mh,Kadogoo aliahidi kuhakikisha wanasimamia fedha hizo ipasavyo ili kufanikisha malengo ya serikali katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha thamani ya majengo na Fedha zinaendana.

Kwa upande wake Kaimu Mhandisi Ujenzi Wilaya ya Monduli Mhandisi Lugano Mwakalinga alibainisha kuwa katika ujenzi wa Shule hiyo kuanzia hatua ya msingi watalazimika kutumia zege la nondo kutokana na aina ya udongo wa eneo hilo kutokuwa nzuri.

"Tutafanya engineering judgment pia baada ya kazi kuendelea kufanyika lakini hapa tunaona tuna aina tofauti ya udongo kwa juu ambayo ni black cotton soil ambayo siyo nzuri kwa ujenzi hivyo kadili tutakavyoendelea kushuka chini tunaweza kuangalia namna ya kubadilisha tabia ya udongo wa hapa Site ili tuweze kubebesha mzigo wa jengo"aliongeza kusema Mhandisi Mwakalinga.

Hata hivyo Diwani wa Kata ya Lepurko Mh,Yonas Masiaya aliishukuru serikali iliyopo madarakani kwa kuwapa fedha hizo na kusema imejibu kiu ya wananchi wa Kata hiyo ya kupata Shule ya Sekondari na kuwaomba wananchi wa Lepurko kuendelea na michango ya ujenzi wa nyumba ya walimu pamoja na mwabweni kulingana na makubaliano yaliyojiwekea.

Share To:

Post A Comment: