Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema ili Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa iendelee kupata Hati Safi katika kaguzi zote kila mwaka kama ambavyo umekuwa ni utamaduni wa Halmashauri hiyo ni vema kudumisha ushirikiano chanya baina ya Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa Halmashauri, Viongozi na Wadau mbalimbali wa Halmashauri.

Senyamule ameyasema haya leo tarehe 13 Julai 2023 Wilayani Kondoa katika mfululizo wa vikao maalumu vya Baraza la Madiwani kwa lengo la kujadili hoja za Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni, 2022.

“Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa ilikuwa na jumla ya hoja 51 (18 zimefungwa bado 33) maagizo 4 ya Kamati ya LAAC ambayo kati ya hayo, maagizo 2 yapo katika hatua ya utekelezaji na magizo 2 bado halijatekelezwa. Kutokana na uwepo wa hoja hizo na maagizo ya kamati ya LAAC, Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa chini ya usimamizi wa Baraza la Madiwani inapaswa kuweka mkazo mkubwa kujibu hoja zote badala ya hoja za hivi karibuni na Maagizo ya Kamati ya Hesabu za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (LAAC)” Senyamule amesisitiza.

Amesema ili kuondokana na changamoto ya Halmashauri kuwa na hoja nyingi zisizofanyiwa kazi ameagiza Kamati ya Fedha ambayo inakutana kila mwezi kuwa na agenda ya kudumu ya kujadili mwenendo wa ujibuji wa hoja za ukaguzi za Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri na zile zinazotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuchukua hatua stahiki pale inapobainika kuwa Menejimenti imefanya uzembe katika kufanyia kazi hoja za ukaguzi na maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa.  

“Kuna uzembe wa watu kutomaliza hoja kwa maksudi naamini mkiweka mkakati wa pamoja hoja zote zitafutwa na Kondoa bila hoja inawezekana endapo mtatumia ipasavyo vikao vya kamati ya Ukaguzi” Senyamule amesisitiza.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imebainisha changamoto za usimamizi wa miradi na miradi kutokukamilika kwa wakati ikiwemo jengo la ofisi la utawala, ujenzi usioridhisha wa vyumba vya madarasa, ujenzi wa jengo la zahanati ya kijiji cha Haire kutekelezwa bila ya kuwa na makisio ya gharama.

“Naelekeza Menejimenti kuhakikisha miradi hii inakamilika na kutumika na taarifa ya utekelezaji niipate 30/09/2023. Kondoa kuna shida ya utekelezaji wa miradi, Jipangeni upya, hakikisheni miradi ya SEQUIP mnakuwa wa kwanza!” Senyamule amesisitiza.

Aidha, Senyamule ametoa msisitiza kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kuimarisha ukusanyaji wa mapato walau kufikisha Bilioni 2 kwa mwaka na kudhamiria kuvuka lengo la Bilioni 1.3 zilizopangwa.

Kupitia kikao hicho maalumu cha Baraza la Madiwani Senyamule pia ametumia hadhara hiyo kusisitiza suala la elimu, mazingira na kilimo na kuagiza kuwa ni agenda ya kudumu katika vikao ngazi zote.

“Elimu ni agenda ya kudumu, ni lazima watoto waende shule na muwataje 55wote wanaotoroka na kuwachukulia hatua wazazi wasiopelekea watoto shule. Kila ijumaa tuwe tunapata taarifa za watoto kwa watendaji wa Kijiji na Kata wana Kondoa tulivalie njuga suala hili”

Nae Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Khamis Mkanachi amesema kuwa Hoja zinazozalishwa zinajibika na amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Bw. Shaban Millao kuandaa bango kitita na mkakati wa kuzimaliza hoja hizo.

Share To:

Post A Comment: