MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdurhaman Kinana, amezungumzia mjadala wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam huku akiweka wazi kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoingoza haiwezi kuuza bandari hiyo na kuhoji Rais auze bandari kwa maslahi yapi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mkendo Musoma Mjini Kinana alianza kwa kueleza kuwa liko jambo la bandari linazungumzwa na mjadala mkubwa, unaendelea kuwa mrefu, mjadala mpana.

“Nataka niwahakikishie msiamini kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyekula kiapo eti atafanya jambo ambalo halina maslahi na nchi. Haiwezi kutokea, Rais ambaye tangu amechukua usukani amefanya mambo mengi mazuri, kwa nini aende kuuza bandari, sababu ni ipi?

“Ili apate nini, ili iweje na ukisikiliza huu mjadala usikilizeni kwa makini na mmeshausikiliza, wote tunaoutetea, wanaopinga pamoja na wanaokosoa hakuna anayesema kwamba kusiwe na uwekezaji hata mmoja kwani wote wanakubali kwamba kuna haja ya kuwekeza  na lengo ni moja tu kuongeza ufanisi na kuongeza mapato.

“Serikali imesema tunakwenda kufanya kazi hii kwa nia njema ya kuongeza ufanisi, kuongeza mapato tuweze kufanya shughuli nyngi zaidi za maendeleo. Wamejitokeza watu wameanza kuhoji, wako wanaohoji kwa nia njema ya kujenga ya uzalendo, hatuwezi kusema kila anayehoji anania mbaya,” alisema.

Aliongeza wako wanaotetea mkataba na wametoa ushauri mzuri, serikali imesema itapokea kila ushauri utakaotolewa, Chama Cha Mapinduzi kimesema serikali isikilize, kwa hiyo serikali inasikiliza ushauri, inasikiliza hoja, haya yote yatafanyiwa kazi, haiwezekani Rais akapuuza haya yote.

“Kiongozi mzuri ni yule ambaye panapotokea ubishani, watu wanabishana na hoja mbalimbali znatolewa anatulia, anasikikiza.

“Anachofanya Rais ni kuwa mtulivu kusikiliza kila hoja kuchambua kila hoja, kutathimini kila hoja, ili muda utakapofika tupate uwekezaji ulio bora zaidi kwa manufaa ya Watanzania. wako waliopeleka mjadala huu katika udini, wengine katika muungano Bara na Visiwani, hakukua na sababu,”alisema Kinana.

Alifafanua kuwa uwekezaji huo ni wa kiuchumi hivyo unatakiwa kujadili kwa hoja,hoja itasikilizwa, hoja yako itajibiwa , pale itakapotakiwa kufanyiwa kazi itafanyiwa kazi kwa maslahi mapana ya nchi.

“Sasa niseme yafuatakayo hakuna anayekataa ,wale wanaopinga na wanaonga mkono, hakuna anayekataa uwekezaji , Serikali inaendelea kusiliza hoja ,maoni na hofu zinazotolewa.

“Chama chetu kimeagiza kwamba wananchi wasikilizwe kwa kila ngazi , kwa kila sehemu, Serikali inaendelea kusikiliza.Sina mashaka hata kidogo kwamba Rais atatoa uamuzi wa busara katika jambo hili na hata uamuzi huu alipoufikia kuwekeza katika  Bandari ni kwa sababu moja tu ya maslahi mapana ya watanzania na nchi sio kwasababu nyingine yoyote.

“Najua tuko watu wengi tuko vyama vingi ndio wakati muafaka sasa likitokea jambo kila mtu anatatafuta namna ya kulitengeneza kwa namna ambayo linakuwa na manufaa kwake. Kwa hiyo ukipiga kelele sana nchi imeuzwa …imeuzwa …imeuzwa ungependa watu waamini kwamba imeuzwa.

"Hakuna bandari inauzwa, inauzwaje? kwanini iuzwe ?Bandari ya Musoma hapa inauzwaje”, kwa bei ipi ? kwasababu ipi? Ili iwe vipi hakuna sababu, naomba tuwe watulivu. Naomba tuwe na imani na Serikali yetu tuwe na imani na Rais wetu ,tumuamini kwamba kila jambo analofanya ni kwa maslahi ya Taifa letu .







Share To:

Post A Comment: