NA DENIS CHAMBI, TANGA.

MAMLAKA ya usimamizi wa wanyama pori Tanzania 'TAWA' imewataka wananchi  waliopo karibu na hifadhi za wanyama kujiepusha na vitendo vyovyote vya ujangiri wa wanyama katika hifadhi na maeneo mbalimbali hapa nchini  huku matukio ya ujangiri yakielezwa kupungua kwa sasa hii ikichangiwa na Elimu iliyokuwa ikitolewa.

Rai hiyo imetolewa na Ofisa Mhifadhi mwandamizi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama pori Tanzania 'TAWA' Proches Rongoma wakati wakishiriki maonyesho ya 10 ya Biashara na Utalii yanayofanyika mkoani Tanga kila mwaka ambapo amesema kuwa hivi karibuni waziri wa Mali asili na Utalii Mohammed Mchengerwa alizindua mpango kabambe utakaosaidia kwa kiasi  kikubwa kuwadhibiti wale wote waliokuwa wakikiuka sheria za kuuwa wanyama pori bila kibali maalum.

"Suala au kitendo chochote cha kuuchukua mali ya wanyama pori bila kibali huo ni ujangiri na ujangiri upo wa aina tofauti upo wa kibiashara na wa chakula kuna watu wanao uwa wanyama kwa ajili ya chakula na kwaajili ya kufanya Biashara  mamlaka ya wanyama pori Tanzania inapenda kuwasihi Sana watanzania wajue kwamba wao ndio wahifadhi wa kwanza wa wanyama pori wa nchi hii"

"Serikali yetu imeleta mfumo wa kupatikana kwa nyama za wanayama. pori katika bucha kwahiyo hakuna sababu ya kusema mtu anawinda ili apate kitoweo kwahiyo tuna mfumo unaokubalika ambao unakuruhusu vinginevyo utakutwa na mkono wa Sheria  hivyo Ni vyema watanzania wajiepushe na ujangiri wa aina yeyote ile" alisema Rongoma

Aidha aliwataka Wananchi wanaoishi karibu na hifadhi mbalimbali hapa nchini kutoa taarifa kwenye Mamlaka husika na kujiepusha kujichukulia hatua mkononi pale wanyama pori wanapokuwa wamevamia katika maeneo ya shughuli za kibinadamu,

"Yapo baadhi ya maeneo yenye changamoto za Wanyama pori kutoka hifadhi mbalimbali kutoka nje ya hifadhi na kwenda kuvamia maeneo ya shughuli za kibinadamu Kama kilimo na makazi , ninachoomba Wananchi mnapoona wanyama pori msiwasogelee karibu na msichukue hatua mkononi ni hatari Sana nivyema mkatoa taarifa kwenye Mamlaka husika"alisisitiza Rongoma

Awali akizungumza  afisa mhifadhi daraja la pili kutoka Mamlaka hiyo Veronica Mollel aliwasisitiza na kuwahimiza watanzania kuendelea kufanya utalii wa ndani katika hifadhi mbalimbali zilizopo hapa nchini ili kujionea vivutio na kujifunza amali mbalimbali zilizopo.

Alisema kuwa kuzinduliwa kwa Royal Tour iliuofanywa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kumekuwa na muamko mkubwa wa watalii sii tu wageni kutoka mataifa mbalimbali bali  hata watanzania wamehamasika na kujitokeza kujionea vivutio huku ushiriki wa wanawake katika sekta mbalimbali ukiongezeka.

"Tanzania tuna vivutio mbalimbali  ushiriki wa wanawake katika sekta mbalimbali za utalii umekuwa ni mkubwa  wapo kwenye doria, kuongoza watalii niwasihi watanzania wote kuwa mabalozi wa rasilimali zetu za Wanyama pori" alisema Mollel.

Maonyesho ya biashara na utalii ambayo hufanyika kila mwaka mkoani Tanga yakishitikisha makampuni, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali  mwaka huu 2023 yamebebwa na kauli mbiu ya "Kilimo, viwanda  utalii na madini  ndio msingi wa maendeleo ya kiuchumi"


Afisa mhifadhi daraja la pili kutoka Mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori Tanzania 'TAWA'   Veronica Mollel akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao kuhusu maonyesho ya 10 ya biashara na utalii yanayofanyika katika viwanja vya Mwahako jijini Tanga .

 
 
Baadhi ya wanachi wa jiji la Tanga waliojitokeza katika maonyesho ya biashara na utalii yanayofanyika katika viwanja vya Mwahako wakiangalia baadhi ya wanyama wanaopatikana katika hifadhi mbalimbali hapa nchini wakiwa wapo kwenye mabanda ya maonyesho hayo.



 

Share To:

Post A Comment: