WATANZANIA Wametakiwa kutumia maonesho ya 47 ya biashara 'Sabasaba' kupata elimu na fursa katika sekta ya Madini ili waweze kunufaika na sekta hiyo kwa kushiriki katika uchimbaji wa Madini, kutoa huduma na kuuza bidhaa katika sekta hiyo.


Hayo yameeelezwa leo jijini Dar es Salaam na Kamishina na Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga alipotembelea Banda la Wizara ya Madini na taasisi zake zilizokutanishwa kwa pamoja na taasisi ya TanzaKwanza kwa kushirikiana na TANTRADE.

Amesema, sekta ya Madini ni muhimu na imekuwa ikichangia Fedha za kigeni hivyo Wizara imeweka nguvu kubwa katika maonesho hayo ili wananchi waweze kufahamu na kunufaika na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

"Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameona kuna umuhimu wa kufanya maonesho haya kwa nguvu kubwa sana ili watu waweze kujua hizi fursa zinazopatikana katika Sekta ya Madini," amesema Dkt. Mwanga.

Ameongeza kuwa, Sekta ya Madini inamchango mkubwa kwenye upatikanaji wa fedha za kigeni ambapo zaidi ya asilimia 50 ya fedha zote za kigeni zinazopatikana nchini zinachangiwa na mauzo ya Madini nje ya nchi.

"Sekta ya Madini inakuwa kwa kasi na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo mstari wa mbele kuitangaza kimataifa na kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na sekta ya madini kuanzia yanapochimbwa, pamoja na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kuuza bidhaa a huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo ulinzi na chakula" Amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mwenza wa Kampuni ya Tanzakwanza iliyoshirikiana na Mamlaka ya maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE,) katika kuandaa maonesho hayo, Francis Daud amesema katika kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hususani katika sekta za kimkakati watawakutanisha na wadau kutoka nchi 123 na kujadili fursa na changamoto ili kwenda mbele zaidi na watanzania kunufaika na rasilimali za Taifa.

Amesema, katika maonesho hayo TanzaKwanza imewakutanisha wadau wa sekta za Madini na TEHAMA na wataendelea kushirikiana na wadau, sekta binafsi na Serikali kwa ujumla katika kuhakikisha sekta za kimkakati zinaleta tija kwa Taifa na watanzania kwa ujumla.

Pia ameipongeza Wizara ya Madini na Taasisi zake pamoja na wadau kwa kupewa kipaumbele katika maonesho hayo na wizara.

Aidha Meneja wa Mawasiliano na Uhamasishaji kutoka Chemba ya Migodi Muki Msami amesisitiza ushiriki wa Kampuni kubwa na za kati za uchimbaji kushiriki katika makongamano mbalimbali ya madini ili kutangaza fursa mbalimbali zilizopo katika migodi yao.

Dkt. Mwanga ametembelea mabanda ya Taasisi za Wizara ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) pamoja na banda la Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM), Peak Rare Earths, Tanzania Chamber of Mines, Jitegemee Holdings Ltd, Yaya Resources, Mkonya Investment Ltd, Mining Services Ltd ili kujionea shughuli zinazofanywa na kampuni hizo.


Kamishina wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga  akitembelea na kuona utendaji kazi wa mabanda ya Wizara ya Madini na Taasisi zake katika maonesho ya 47 ya biashara 'Sabasaba' yanayoendelea jijini Dar es Salaam.








Share To:

Post A Comment: