Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatuma Mganga akizungumza jana  wakati akifungua mafunzo yanayohusu usimamizi bora wa shughuli za Halmashauri kwa Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida. Kushoto ni Naibu Meya Jiji la Arusha, Veronica Mwelange.

Na Dotto Mwaibale, Singida

KATIBU Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatuma Mganga amesema suala la kuleta maendeleo ya nchi sio la Rais Samia Suluhu Hassan peke yake bali ni la wananchi wote.

Dk. Mganga ameyasema hayo jana wakati akifungua mafunzo yanayohusu usimamizi bora wa shughuli za halmashauri kwa Wenyeviti wa Halamashauri na Mameya yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida.

"Suala la kuiletea nchi maendeleo sio la Rais peke yake bali ni la kila mmoja wetu mahali popote alipo na hii dhana ya kusema ni jukumu la mkuu wa nchi halina mashiko," alisema Dk. Mganga.

Alisema mafunzo hayo yamekuja wakati sahihi ambapo taifa letu chini ya Rais Samia linapambana  kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kasi.

Dk. Mganga aliongeza kusema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo kwenye maeneo muhimu ya uongozi na utawala bora, namna ya kubuni vyanzo vipya vya mapato na usimamzi wa makusanyo ya halmashauri, usimamizi bora wa miradi ya maendeleo kwa kutumia mfumo wa force account pamoja na upangaji, ufuatiliaji na tathimini ya miradi ya maendeleo.

"Mafunzo haya ni muhimu sana kwenu wenyeviti wa halmashauri na mameya kwa kuwa yanalenga kuwaimarisha katika kuhakikisha kuwa mnatekeleza majukumu yenu ipasavyo ili kuleta tija na matokeo makubwa.

Mkurugenzi wa TIA Kampasi ya Singida,  Dk. James Mrema akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA (CEO), Profesa William Pallangyo alisema wameandaa mafunzo hayo lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wenyeviti na mameya juu ya namna ya bora ya kuongoza na kuendesha shughuli za halmashauri hasa kwenye masuala yanayohusu ukusanyaji wa mapato na mambo mengine.

"Katika mafunzo haya tunategemea wenyeviti wa halmashauri na mameya waweze kwanza kujua majukumu yao ukizingatia kuwa wao ndio wasimamizi wakuu katika maeneo yao na kuwa kutakuwa na mada mbalimbali zitakazotolewa na baada ya mafunzo hayo waweze kurudi katika vituo vyao vya kazi na kufanyakazi kwa umahiri mkubwa," alisema Dk.Mrema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi , Idrisa Omari Mgaza, akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwao kwani yatawaongezea ujuzi ambao wataenda kuhufanyia kazi katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Mkurugenzi wa TIA Kampasi ya Singida,  Dk. James Mrema akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA (CEO), Profesa William Pallangyo wakati akitoa neno la shukurani kwa Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga ambaye alikuwa mgeni rasmi wa kufungua mafunzo hayo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi , Idrisa Omari Mgaza, akizungumza kwa niaba ya wenzake baada ya kufunguliwa kwa mafunzohayo.
Mafunzo yakifunguliwa.
Taswira ya mafunzo hayo.
Watoa mada katika mafunzo hayo wakimsikiliza mgeni rasmi.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: