NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deogratias Ndejembi amesema Serikali haina posho ya mazingira magumu kwa walimu lakini iko katika maandalizi ya mwongozo wa ulipaji posho ya masaa ya ziada.

Pia amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara kufanya msawazo wa walimu kutoka shule zenye ziada na kuwapeleka katika shule zanye upungufu zaidi.

Ndejembi ameyasema hayo jana bungeni wakati wa kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Kunti Majala (CCM).

Katika swali lake Majala alitaka kujua ni lini serikali itatoa posho ya mazingira magumu kwa walimu waliovijijini hususani walimuwa wanawake.

Akijibu swali hilo, Njejembi alisema Serikali inaweka uwezeshaji kwa walimu kwa kujenga nyumba karibu na shule na kuwa hakuna posho mahususi ya mazingira magumu inayotolewa.

“Kwa sasa tunaendelea na kazi ya kuandaa mwongozo wa ulipaji posho kwa masaa ya ziada.”

Katika swali la nyongeza, Majala alitaka kujua mpango wa serikali wa kupeleka walimu wa kike katika shule za sekondari na msingi wilayani Chemba.

Akijibu swali hilo, Ndejembi alisema Serikali imekuwa ikitoa ajira ili kukabiliana na upungufu wa walimu shuleni unaotokana na walimu kustaafu, kuacha kazi, kufukuzwa, kufariki na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa.

Alisema kwa mwaka 2021/22, Serikali imeajiri jumla ya walimu 26,598 wakiwemo 16,640 wa shule za msingi na 9,958 wa shule za sekondari.

Ndejembi alisema kwa upande wa ajira zilizotangazwa 2021/22, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilipata walimu 46 wakiume na walimu 49 wa kike kwa shule za msingi na sekondari.

“Ofisi ya Rais-TAMISEMI imetoa maelekezo kwa makatibu tawala wa mikoa wote Tanzania Bara kufanya msawazo wa walimu kutoka shule zenye ziada na kuwapeleka katika shule zanye upungufu zaidi kwa kuzingatia jinsia ili kuwa na uwiano wa walimu wa kike na kiume kwenye shule zetu mbalimbali.”


Share To:

Post A Comment: