Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaasa wananchi kuacha tabia ya kuwashambulia Askari wa Uhifadhi pindi wanapokamata wahalifu huku akiwapongeza Askari wa Uhifadhi wa Manyara kwa kuzingatia maelekezo aliyoyatoa kwa askari wote wa uhifadhi nchi nzima ya kuwataka kutumia busara , weledi na  kuzingatia sheria wakiwa kwenye doria badala ya kutumia nguvu zisizohitajika.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Mei 23, 2023 wakati alipoongea na Vyombo vya Habari   kuhusu  tukio la uvamizi wa majangili katika eneo la Hifadhi la Ziwa Manyara  waliokamatwa  na Askari wa uhifadhi bila kutumia nguvu wala silaha ambapo  baada ya kukamatwa wakiwa ndani ya ziwa hilo, majangili  walio karibu na boti ya doria waliwasaidia watuhumiwa na kutaka kuzamisha boti hiyo.

Amesema baada ya purukushani hiyo majangili  wenzao wapatao 40  waliokuwa karibu na tukio walikuja na kuanza kuwashambulia Askari wanne waliokuwa  kwenye boti na kuharibu mashine ambapo askari hao walijipa ujasiri wakapiga makasia  na hatimaye kutia nanga katika eneo la Nyati.

Ameongeza kuwa baada ya kuweka nanga katika eneo la Nyati, eneo ambalo askari mmoja wa uhifadhi aliuawa kwa kushambuliwa na Nyati katika siku za hivi karibuni, majangili hao waliendelea kuwashambulia lakini askari hao waliendelea kutumia  busara na  hawakuweza kutumia silaha walizonazo.

“Kwa kuwa  nilishatoa maelekezo kwa askari wote wa uhifadhi nchi nzima  kutotumia nguvu wakati wa ukamataji wahalifu hata inapokuwa ndani ya hifadhi, watumie busara na weledi na pamoja kwamba askari hawa walikuwa na silaha hawakutumia nguvu wala silaha hali hii ilipelekea majangili hao kushirikiana  na wenzao  kuwavamia na kuwateka askari na wale watuhumiwa ambao walikuwa wamekamatwa na kutiwa pingu.” Amefafanua 

Ameeleza kuwa  majangili hao walifanikiwa kuwatorosha watuhumiwa  wakiwa chini ya ulinzi na wakiwa na pingu ambapo askari wa uhifadhi waliomba msaada mara moja  kwa askari wenzao na wakatoa taarifa kwa jeshi la polisi na polisi walipofika walifanikiwa kuwaokoa  askari wa uhifadhi waliokuwa wakishambuliwa na kutaka kuuawa na majangili hao.

Amesema baada ya  tukio hilo majangili  walikusanyika tena na kuanza kuvamia  kwenye Ofisi ya  vijiji  na kutaka kuingia kwenye lango la Ofisi za Hifadhi ya Manyara ambapo amesema  Jeshi la Polisi walitumia takribani masaa manne  kuzuia vurugu hizo ili wasiingie ndani ya Hifadhi  kufanya  uhalibifu au matukio mengine ya kiuhalifu ambapo  pia walitumia mabomu ya machozi.

Amesema hata baada ya kutumia mabomu ya machozi bado vurugu ziliendelea na kupelekea mtu moja kufariki.

Akisimulia  kwa uchungu Waziri Mchengerwa  amesisitiza kuwa tukio hilo ni la kusikitisha kwa kuwa haya yote yasingeweza kutokea kama wananchi wangetii  sheria, aidha  askari  wote wa hifadhi wangeweza kuzama kwenye maji baada ya kushambuliwa na majangili na wananchi kuanza  kuchukua sheria mkononi kwa kuwashambulia wahifadhi bila kuogopa na kuwatorosha watuhumiwa waliokamatwa kwa kufuata taratibu bila  kuwapiga wala kutumia silaha walizokuwa nazo.

 Amesema Serikali imeandaa  maeneo mengi kwa ajili ya matumizi mbalimbali  ikiwa ni pamoja na shughuli za uhifadhi, kilimo, ufugaji na uvuvi ambapo  wananchi wangeweza kuyatumia kwa  kuzingatia sheria ambazo zimetungwa na wawakilishi wao  bungeni kwa miaka  mingi kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye badala  ya kuwa sehemu ya uhalifu.


“Sisi kama Serikali tunatamani kuona kila mwananchi awe na furaha lakini tunawaomba watanzania, hatupaswi kugombana kwa kuwa maeneo ni mengi, naomba sana wananchi wafuate sheria, iwapo  kila mtanzania akitii sheria ambazo tumezitunga sisi wenyewe hakutakuwa na mivutano yoyote baina ya wananchi na wahifadhi, na sisis tumejitahidi katika kipindi hiki kifupi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wetu, tunaendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki katika uhifadhi kwa kuwa wananchi ndiyo wahifadhi namba moja” Amesisitiza

Aidha amewataka wahalifu wote walioshiriki katika tukio hili kujitokeza mara moja kwenye jeshi la polisi kwa kuwa tayari taarifa ilifatolewa   kabla ya tukio hilo kuwa kubwa ambapo amelishukuru jeshi la polisi kwa kuokoa askari wa uhifadhi ambao ni watoto wa watanzania  ambao wanafanya kazi kubwa  ya uhifadhi wa raslimali kwa faida ya taifa zima.

Kufuatia  vurugu hizo Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia watu 12 wanaodaiwa  kufanya uhalifu na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwasaka  vinara wa vurugu hizo ambapo pia amesisitiza  kwa wananchi kuzingatia sheria  za nchi  na  kuacha  tabia za uvuvi haramu.
Share To:

Post A Comment: