MOROGORO

Akizungumza katika Mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa Mameneja wa Mikoa TANROADS Nchini na Wakuu wa Idara na Divisheni TANROADS Makao Makuu, Mkufunzi wa mafunzo na Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini amewataka Watendaji hao kuhakikisha kuwa Mawasiliano yote yanayofanyika kwa njia ya TEHAMA yanazingatia Usalama na Sheria za Nchi.


Akiwasilisha mada za kuwajengea uwezo Watendaji hao kuhusu Utawala bora, Mawasiliano na Uhusiano, Itifaki na Ustaarabu Mafunzo yaliyofanyika Mjini Morogoro Sagini amesema kuwa licha ya kuwa TANROADS imekuwa ikifanya vizuri katika kutekeleza majukumu yake na kuwaletea maendeleo Wananchi kupitia miradi mbalimbali bado elimu inahitajika kujua Sheria,Kanuni na Miongozo ili kuwa na Uwazi na Uwajibikaji katika Taasisi hiyo.


“Kila mtu anapaswa kuzingatia na kuheshimu Katiba ya Nchi, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yake kuzingatia haki, kuepuka ubaguzi na upendeleo. Viongozi wanapaswa kuwa karibu na Wananchi wanapaswa kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maamuzi pamoja na utendaji kazi wao. Aidha maamuzi na vitendo vya Viongozi katika utekelezaji wa majukumu lazima yafanywe kwa uwazi ili Wananchi waweze kujua kinachoendelea katika maeneo yao.” Alisema Sagini


Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti baadhi ya Mameneja wa TANROADS akiwemo Mhandisi Motta Kyando kutoka katika Mkoa wa Kilimanjaro amesema kuwa mafunzo haya ni muhimu kwani yanasaidi katika kuboresha utendaji kazi na kufanya mawasiliano ya kimkakati ili kuboresha utendaji kazi katika Taasisi.


Kwa upande wao baadhi ya Wahandisi kutoka Makao Makuu ya TANROADS wamesema kuwa mafunzo haya ni muhimu kwani yanawasaidia Watendaji katika kuzitambua haki na wajibu wa Watumishi wanaowasimamia na kwa namna gani wanaweza kuboresha mahusiano katika Taasisi.


Serikali kupitia Taasisi mbalimbali za Mafunzo zimeendelea kutoa mafunzo elekezi kwa Viongozi, Watendaji na Watumishi wa Serikali ili kutambua mipaka yao ya kazi na kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utendaji kazi wao.Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: