Na; Elizabeth Paulo, Dodoma


Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limefanikiwa kuwadhibiti majambazi wanne wakiume ambao majina yao bado hayajatambulika wenye umri kati ya miaka 25 mpaka 30.



Kauli hiyo Imetolewa leo na kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma Martin Otieno mbele ya waandishi wa Habari alipokua akieleza Hali ya ulinzi na usalama kwa Mkoa huku akisema majambazi hao walikuwa katika harakati za kufanya tukio la unyang'anyi wa kutumia silaha mnamo April 25 majira ya ya saa3 usiku katika mtaa wa mwangaza -Kisasa kata ya Makulu.



Kamanda Otieno amesema majambazi hao walivamia nyumbani kwa Bi. Edna Joseph Kashashari (41), mfanyabiashara, mkazi wa Kisasa wakiwa wamevaa barakoa usoni na kufanikiwa kunyang'anya pesa taslim 1,100,000/= simu ya Samsung moja na simu ndogo tatu baada ya watu hao kumtishia kumkata mapanga ndipo mhanga alipiga kelele za kuomba msaada.


“Baada ya mhanga kupiga kelele za kuomba msaada ambazo zilisikika kwa majirani na majirani hao kutoa taarifa kwa askari wa waliokuwa doria eneo hilo ambao walifika kwa haraka na kuwakuta watu hao ambao walijihami kwa kutaka kuwashambulia askari kwa mapanga na askari hao kujibu mapigo kwa kuwafyatulia risasi ambazo ziliwajeruhi watuhumiwa hao maeneo mbalimbali ya miili yao,”amesema.



Aidha ameongeza kuwa majambazi hao walijificha nyuma ya ukuta wa fensi na kuruka ukuta huo na kwenda kumvizia Edna Joseph Kashashari wakati anataka kufunga mlango wa nyumba na kumtishia kumkata na mapanga kisha kumpora vitu hivyo.


Amesema majambazi hao wanne walifariki dunia wakiwa wanapelekwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kwa matibabu.


“Kwasasa hali ya mkoa ni shwari na jeshi la polisi lipo makini kuhakikisha hali ya amani inaendelea kuwepo,”ameongeza


Kamanda Otieno ametoa wito kwa wageni wote wanaoingia mkoani Dodoma kuacha kufanya vitendo vya kihalifu kwani mkoa wa Dodoma umeimarisha Ulinzi na Usalama.

Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: