Na Mwandishi Wetu

NDOTO za vijana wa Tanzania wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi kwa mwaka wa masomo 2026/2027 zimeingia hatua muhimu baada ya Global Education Link kuwakutanisha wanafunzi hao pamoja na wazazi na walezi wao kwa ajili ya kuhakiki nyaraka na kukamilisha maandalizi ya safari.

Kikao hicho kilichofanyika katika Makao Makuu ya Global Education Link, Dar es Salaam, kililenga kuhakikisha kila mwanafunzi anakuwa na nyaraka sahihi, taarifa za kutosha na maandalizi muhimu kabla ya kuondoka nchini kwenda kuanza masomo.

Miongoni mwa mambo yaliyopitiwa katika kikao hicho ni pamoja na nyaraka za visa, barua za udahili, fomu za uthibitisho wa malazi, maandalizi ya safari pamoja na maelekezo ya namna ya kuishi na kusoma katika mazingira mapya nje ya Tanzania.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, alisema lengo kuu la kikao hicho ni kuhakiki na kukamilisha nyaraka muhimu za wanafunzi, kujibu maswali ya wazazi na kuhakikisha changamoto zinazoweza kuchelewesha safari zinapatiwa ufumbuzi mapema.

Mollel alisema moja ya mambo muhimu ambayo wazazi, walezi na wanafunzi wanapaswa kuzingatia baada ya kuchagua chuo ni kujiridhisha kuhusu utambuzi wake wa kisheria.

Alisema hata kama mwanafunzi ameshauriwa au kupewa chuo kupitia Global Education Link, bado mzazi au mlezi ana wajibu wa kuhakikisha taasisi hiyo inatambuliwa rasmi na mamlaka zinazohusika.

“Hata kama chuo umepewa na Global Education Link, mzazi unapaswa kujiridhisha kuhusu utambuzi wake. Njia sahihi ni kupata uthibitisho rasmi kutoka katika mamlaka ya Serikali inayosimamia vyuo vikuu,” alisema Mollel.

Aliongeza kuwa barua rasmi ya uthibitisho kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ndiyo inayomwezesha mzazi au mwanafunzi kuwa na uhakika kuwa chuo kilichochaguliwa kinatambuliwa kisheria.

Mollel alisema hatua hiyo ni muhimu kwa sababu inalinda maslahi ya mwanafunzi na kuhakikisha shahada, stashahada au sifa nyingine atakazopata baada ya kuhitimu zinaweza kutambuliwa na mamlaka husika nchini.

Aliwataka wazazi kutoridhika na taarifa zinazopatikana kupitia mitandao ya kijamii, matangazo au maelezo yasiyo rasmi pekee, bali kufuata utaratibu unaotambuliwa na Serikali kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Kwa mujibu wa Mollel, safari ya masomo nje ya nchi haiishii katika kupata nafasi ya kujiunga na chuo pekee, bali inahitaji maandalizi kuhusu visa, malazi, usafiri, usalama, sheria, utamaduni wa nchi husika na uwezo wa mwanafunzi kuishi kwa nidhamu na uwajibikaji.

Alisema Global Education Link imeweka utaratibu wa kuwaongoza wanafunzi na wazazi wao hatua kwa hatua, kuanzia uchaguzi wa kozi na chuo, maombi ya udahili, upatikanaji wa barua ya kujiunga, uthibitisho wa chuo, maombi ya visa, maandalizi ya malazi hadi kufanikisha safari.

Mollel pia aliwataka wanafunzi kutumia fursa hizo kwa nidhamu, kusoma kwa bidii na kutambua kuwa wanapokuwa nje ya nchi wanawakilisha familia zao na Tanzania.

Kwa upande wao, wazazi na walezi walioshiriki kikao hicho walisema wameridhishwa na namna Global Education Link ilivyowahudumia na kuwapatia majibu kuhusu hatua mbalimbali za udahili na maandalizi ya safari.

Mmoja wa walezi hao, Asuba Omary kutoka Zanzibar, alisema alishiriki mkutano huo baada ya kukaribishwa na Ofisi ya Global Education Link Zanzibar.

Omary, ambaye anafanya maandalizi ya kumpeleka mdogo wake kusoma nje ya nchi, alisema kikao hicho kimemsaidia kufahamu mambo ya kuzingatia kabla ya mzazi kuamua kumsomesha mtoto katika chuo kikuu cha nje ya Tanzania.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: