Na;Elizabeth Paulo, Dodoma

Hadi kufikia juni 30, 2022, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umelipa mafao yenye thamani ya Shilingi Bilioni 44.61 kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko kubwa kwa kulinganisha na kipindi cha kabla ya kuanza kwa WCF ambapo malipo ya fidia yalikuwa chini ya Shilingi Milioni 200 kwa mwaka. 


Katika kipindi cha Julai 2022 hadi Desemba 2022, WCF ililipa mafao ya jumla ya Shilingi Bilioni 6.19 kwa wanufaika 1,004 na hivyo kufanya wanufaika wa Mfuko toka kuanzishwa kwake kufikia 10,454 ambao wamelipwa jumla ya Shilingi Bilioni 49.44.  


Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amebainisha hayo wakati wa akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Machi 02, 2023 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma.


Mfuko huo umeendelea kulipa fidia hizo kupambana na umaskini na kufanya malipo endelevu (pensheni) kwa wanufaika ambapo kwa mwezi Juni 2022, wanufaika 1,114 walilipwa kiasi cha Shilingi Milioni 231.39 kwa mwezi huo.


Dkt. Mduma amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imefanya maboresho kadha wa kadha katika kutelekeza andiko maraafu kwa jina la Blueprint. Kupitia WCF."Serikali imetekeleza Yafuatayo ikiwa ni Kushusha kiwango cha mchango toka sekta binafsi hadi kufikia tarehe 13 Juni, 2021 ambapo Serikali ilileta unafuu kwa kutangaza kushusha kiwango cha mchango kwa Sekta Binafsi kutoka asilimia moja (1) hadi asilimia (0.6%) ya michango ya wafanyakazi. Na Julia 2022 Serikali iliendelea kuboresha kwa kushusha zaidi kiwango hicho hadi kufikia asilimia (0.5%) ili kuweka usawa kwa sekta zote yaani Sekta za Umma na binafsi".Alisema Dkt.Mduma


 Amesema Serikali iliendelea kuleta unafuu zaidi kwa waajiri kwa kupunguza kiwango cha kodi ya malimbikizo ya madeni ya michango ya nyuma kutoka asilimia kumi (10%) hadi asilimia mbili (2%) ili kuhamasisha waajiri ambao hawajajisajili waweze kujisajili na watekeleze wajibu wao wa kulipa michango kwa ajili ya kulinda wafanyakazi wao dhidi ya majanga yatokanayo na kazi.


"Sanjari na hayo, Serikali kupitia WCF imetekeleza sera ya msamaha wa riba kwa waajiri waliochelewesha michango tangu Mfuko ulipoanza mwaka 2015 hadi Juni 2022 kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kuondoa mzigo kwa waajiri ambao hawakuweza kulipia wafanyakazi wao kwa sababu mbalimbali".Alisema


Uamuzi wa kushusha viwango vya uchangiaji kwa Sekta binafsi unalenga kumpunguzia mzigo mwajiri ili fedha alizokuwa akitumia kuchangia zielekezwe kwenye maeneo mengine ya uendeshaji wa shughuli zake za uzalishaji. 


Aidha amesema Serikali kupitia WCF imetekeleza sera ya kuongeza kima cha chini cha fidia hadi kufikia shilingi 275,333 kutoka utaratibu wa awali ambao haukuwa na kima cha chini cha fidia kwa mfanyakazi ambaye hakupata ulemavu wa asilimia 100.  


 Ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuendelea kutekeleza wajibu wao kwenye Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi na kwamba Mwajiri ndiye mwenye jukumu la kuchangia kwenye Mfuko wa WCF na ni kosa la jinai kutofanya hivyo na kusema Mfuko huo utakua Imara kwa miaka 30 ijayo hadi 2047.


WCF ni Taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263] kwa lengo la kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaopata ulemavu au kufariki kutokana na magonjwa au ajali zitokanazo na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba yao ya ajira.


Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: