Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel (wa nne kutoka kushoto) akizungumza katika mkutano uliohusu kongamano la fursa la Wanamuziki litakalofanyika kuanzia Mei 22 hadi 27, 2023 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya ElimuViumbe jijini Arusha.

 Na Dotto Mwaibale, Arusha

UMOJA waWana muziki Tanzania (TAMUFO) kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa wameandaa kongamano la fursa litakalofanyika kuanzia Mei 22 hadi 27, 2023 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya ElimuViumbe jijini Arusha.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Arusha leo Machi 24, 2023, Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel alisema kongamano hilo la siku sita lenye kauli mbiu isemayo Twende na Muziki katika Maendeleo ya Taifa Letu litawajumuisha wanamuziki wakongwe, vijana pamoja na wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla.

"Kongamano hili ni la kihistoria ambalo halijawahi kufanyika hapa nchini kabla ya uhuru na baada ya uhuru hivyo haitakiwi mtu kulikosa," alisema Joel.

Joel alisema muziki Umetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi ambapo alimtaja  Mhasisi wa Taifa letu Mwalimu Julias Kambarage Nyerere kuwa aliwatumia wanamuziki katika kuhamasisha maendeleo ya Taifa wakiimba nyimbo zenye ujumbe wa kufundisha na kukemea maovu na kuwatetea waafrika wenzetu kama  Afrika Kusini, Zimbabwe na maeneo mengine ya Afrika.

Alisema hata wakati wa Muungano Mwaka 1964 Nyimbo ziliimbwa kuhakikisha unafana ambapo wanamuziki waliimba nyimbo za kuhamasisha uzalendo, nidhamu kazini pia kukemea vitendo vya rushwa, uhujumu uchumi, walanguzi na wafujaji wa mali ya umma.

"Ndugu zangu muziki una nguvu hata kwenye vitabu vya dini tunasoma kwamba uliweza kuangusha ngome za Jerico hivyo kuna haja ya kuendelea kuhuhamasisha kwa nguvu zetu zote  uendelee  kutuletea maendeleo ya Taifa letu n,"  alisema Joel.

Alisema katika Kongamano hilo tayari wanamuziki kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini, vikundi vya bendi, waimbaji binafsi wameanza kujiandaa kwenda jijini Arusha kushiriki kongamano hilo la kihistoria ambalo limesheheni fursa lukuki kutoka  kwa wadau  mbalimbali wa maendeleo,  Taasisi za kiserikali na za Kiraia ambao watakuwepo kutoa elimu katika nyanja za Sanaa.

Joel alisema kupitia kongamano hilo wanamuziki watapata nafasi ya kufahamiana na wenzao ambao watatoka nje ya nchi na kupata fursa ya kusikia hotuba kutoka kwa viongozi wa Serikali

Aidha Joel alitumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo  ambao wanatoa ushirikiano mkubwa kuhakikisha Kongamano hiloi linafanyika kwa kushirikiana na BASATA na COSOTA ambao watakuwepo kwenye kongamano hilo.

Mkurugenzi wa Makumbusho ya Elimu Viumbe Arusha, Dk. Christina Ngerza, alisema  Makumbusho hiyo imejipanga vizuri kutoa Elimu ya Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni na kuwa wanamuziki ni watu muhimu katika kuhamasisha Maendeleo ya nchi hivyo Makumbusho itaendelea kushirikiana na TAMUFO ili Kuwajengea uelewa Wanamuzi jinsi ya  kuhifadhi urithi wa utamaduni wetu katika nyanja mbalimbali.

Meneja Biashara Maendeleo wa Benki ya NBC Mkoa wa Arusha, Prince Moshi akimwakilisha Meneja wa benki hiyo Mkoa wa Arusha alisema benki hiyo inaunga mkono Juhudi hizo ambapo kupitia kongamano hilo watatoa fursa za Kibenki kuhakikisha Muziki na Wanamuziki wanapata Bima ya Afya na Mikopo na Elimu za Kibenki kwa maendeleo ya Tasinia hiyo.

Mlezi wa TAMUFO Dk.Frank Richard alitoa wito kwa Wanamuziki kujitokeza kwa wingi katika kongamano hilo ambalo litaambatana na kutalii katika hifadhi kwa siku moja ambapo aliwaomba wadau wote kushiriki ili kuunga mkono Juhudi za Serikali yetu ya Awamu Ya Sita za kuutangaza utalii wa nchi yetu.

Mkurugenzi wa Makumbusho ya Elimu Viumbe Arusha, Dk. Christina Ngerza, akizungumza katika mkutano huo.
Meneja Biashara Maendeleo wa Benki ya NBC Mkoa wa Arusha, Prince Moshi (wa tatu kutoka kushoto) akizungumza kwenye mkutano huo.
Mlezi wa TAMUFO Dk.Frank Richard (wa kwanza kushoto) akitoa wito kwa Wanamuziki kujitokeza kwa wingi katika kongamano hilo.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: