Na;Elizabeth Paulo, Dodoma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia sekta ya Afya kwa kushirikiana na Mashirika yasiyo ya Kiserikali inaendelea kuimarisha huduma za Miradi ya Afya ya Macho kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa.


Kauli hiyo imetolewa leo machi 17 Jijini Dodoma na Muuguzi Mkuu wa Serikali Bi. Ziada Sellah Kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe Wakati wa Uzinduzi wa Miradi ya Afya ya Macho kwa ufadhili wa Shirila la CHRISTOFEEL BLINDEN MISSION(CBM) uliofanyika Katika Ofisi za wizara Area D.


Bi. Sellah Ametoa wito kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma kwa upande wananchi wa Tanzania kwa uwiano mzuri.


Uboreshaji wa Huduma pekee hautazaa matunda iwapo wananchi hamtachukua hatua madhubuti za kujikinga na kutumia vituo vyetu vya tiba kufanya uchunguzi na tiba pale inapohitajika. Amesema Bi. Sellah


Ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na Ulemavu wa kutokuona unaozuilika nchini kwa kujitokeza kwa wingi kutumia huduma hizo.


Ninatoa wito kwa kila mwananchi kudhamiria na kujiunga na Mifuko ya Bima za Afya ili kukabiliana na changamoto za garama za kupata matibabu ambapo mwananchi anatumia fedha nyingi wakati wa kuhudumiwa kwa kuwa wakati mwingi ugonjwa humuingia mtu akiwa hajajiandaa, Pamoja na kunuwezesha mtu kurejeshewa afya yake kupitia tiba, Bima ya Afya ni suluhisho pekee kwa ustawi wa wanafamilia na Afya njema itamuwezesha mtu kujumuika kwenye shughuli za kiuchumi na kwa watoto kufuatilia vyema masomo yao chuoni au shuleni. Ametoa wito Bi. Sellah



Kadhalika Ametoa rai kwa watendaji na wasimamilizi wa Huduma za Macho kwenye vituo ambavyo vitapokea vifaa kuzingatia vifaa hivyo vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuingizwa kwenye orodha ya vifaa vya hospitali husika na kutunzwa huku vikifanyiwa matengenezo kinga ili viweze kutoa huduma kwa muda mrefu kwa manufaa ya wananchi.


Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ninapenda kutoa shukrani za dhati kwa shirika la CBM na washirika wake kwa msaada huu ambao utachangia uimarishaji wa huduma za macho kwa wananchi wa Tanzania. Ameshukuru Bi Sellah


Awali akitoa taarifa ya mradi wa macho wa huduma toshelezi na jumuishi za afya ya macho kwa ufadhili wa shirika hilo Mganga Mfawidhi hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Lindi Dkt. Alexander Makalla Amesema kulingana na Shirika la Afya Duniani mkoa huo unakadiriwa kuwa na takribani watu 10,250 wasioona huku watu 41,000 wenye upungufu wa kuona wa kati na wa kiwango cha juu wakati mkoa huo unajumla ya wakazi 1,025,800.


Dkt. Makalla amesema katika kutafuta rasilimali za kuboresha huduma za macho hospitali iliitika wito kutoka wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa huduma za macho kwa kuandaa andiko lililoboreshwa na Mpango huo wa Taifa na kuwasilishwa shirika la Christoffel Blinden Mission (CBM) ili kupata ufadhili.


Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi - Sokoine imepata ufadhili wa shilingi za kitanzania 819,238,062 zinazondelea kutekeleza Mradi wa Toshelezi na Jumuishi za Afya ya Macho katika mkoa wa Lindi kwa miaka minne uliozinduliwa leo kwa Lengo la kuongeza juhudi za kupunguza upungufu wa kuona unaozuilika na kujumuisha huduma msingi na jamii ya afya ya macho ambapo lengo mahususi ni kuimarisha vitengo vya huduma za macho kwa ajili ya utolewaji wa huduma jumuishi za afya ya macho katika mkoa huo.



Kwa niaba ya watumishi wa Hospitali ya Sokoine hususani Idara ya Macho ninapenda Kutoa shukrani za dhati kwa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitiada za kuboresha Miundombinu, Vifaa na Vifaa tiba kwenye hospitali zeti hapa nchini, Pia natoa shukrani kwa Wizara ya Afya kwa msaada mkubwa wa kitaalamu na jinsi mlivyoshughulikia na kuhakikisha Mkataba wa Mradi huu umesainiwa. Aidha tunawashukuru sana wafadhili wetu CBM kwa kutekeleza mradi huu unaoenda kubadilisha maisha ya wananchi wa Lindi na sehemu jirani, Tunaahidi kushirikiana na Wizara ya Afya katika kutekeleza shughuli za mradi huu kwa wakati ili matokeo yake yaweze kufikiwa. Amesema Dkt. Makalla



Naye Mkurugenzi Mkazi wa CBM Tanzania Nesia Mahenge Amesema shirika linatoa kipaumbele katika Afya ya macho kulingana na umuhimu wa macho kwani bila kuwa na macho yanayoona vizuri kutakuwepo na changamoto katika maendeleo ya nchi hata Uchumi wa mtu mmoja mmoja.


Tunazingatia sana kuhamasisha mtoto kuanzia umri mdogo au kabla hajazaliwa Mama/Mzazi azingatie afya bora na mtoto anapozaliwa anafanyiwa uchunguzi toka mapema ili kutambua madhara yoyote kwenye macho na apatiwe huduma tangu mdogo, Kwahiyo tunasema sana suala la kinga kabla ya kutibu na baada ya hapo kwa ambao tayari wanamataizo ya macho tunahamasisha sana kupima macho haijalishi umri kwasababu unaweza ukawa unaona lakini usijue kwa jinsi unavyokwenda kama hupati tiba stahiki ni rahisi sana yale macho kupelekea ukapata upofu wa kutokuona kabisa. Amefafanua Bi. Mahenge



Bi. Mahenge amesema Shirika la CHRISTOFEEL BLINDEN MISSION(CBM) ina zaidi ya Miaka 50 nchini Tanzania tangu kuanzishwa kwake ikiwemo Tanzania Bara na Zanzibar kwa kupitia Taasisi na kushirikiana na Serikali kwa kutoa rasilimali fedha au kuwajengea watu uwezo.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Tiba Dkt. Mwinyi Kondo Amesema Uzinduzi wa Miradi hiyo umeenda sambamba na wiki maalumu ya kuelimisha jamii kuhusiana na shinikizo la macho ambapo maadhimisho ya kimataifa yamebeba kauli mbiu isemayo "Dunia angavu,Tunza uoni wako".



Aidha Dkt. Kondo amesema maadhimisho hayo kwa mwaka huu yanalenga kuinua uelewa wa wananchi kuhusu visababishi na viashiria vya ugonjwa wa shinikizo la macho.


Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho Dkt. Bernadetha Shilio Amesema mikakati ya Serikali ni kutafuta rasilimali katika kuboresha huduma ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu ambapo awali madaktari bingwa wa macho ni pungufu ya 50 lakini mpaka sasa Tanzania inakaribia kuwa na madaktari bingwa wa macho 90 huku Serikali ikiendelea kufadhili madaktari bingwa kwaajili ya kufikisha huduma katika maeneo ambayo hayafikiwa.



Mkoa wa Lindi ni mmoja ya mikoa ambayo ilikua na uhitaji mkubwa wa huduma za afya ya macho huku mikoa ya Kigoma na Tabora pia ikiwa na idadi ya wagomjwa wengi wenye matatizo ya afya ya Macho.


Miradi hii ina jumla ya thamani ya shilingi za kitanzania Bilioni 1.47 ambapo shilingi 646,850,800 ni kwaajili ya Mfumo wa Huduma za Macho huku shilingi 819,238,062 ikiwa kwaajili ya huduma Jumuishi za macho kwenye mkoa wa Lindi

Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: