BODI ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeipongeza TFS kwa kuboresha miundombinu na huduma za utalii katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia ya Pugu Kazimzumbwi uliopo Kisarawe mkoani Pwani na kuwezesha maeneo yake yote ya utalii kufikika kwa wepesi katika vipindi vyote vya mwaka.
Baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo pia walipata fursa ya kutembelea ofisi za mkoa wa Pwani, ambapo pamoja na mambo mengine wamekutana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe Abubakar Kunenge na kujadili kuhusu utekelezaji wa shughuli za uhifadhi kwa mkoa huo.
Wakati wa ziara hiyo iliyokuwa na wajumbe wawili, CPA. Bahati Lucas Masila, Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais na Adv. Piensia Christopher Kiure, Mkurugenzi wa Uhusiano, Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya TFS, na baadhi ya wataalamu kutoka TFS,wajumbe wa bodi walifurahishwa na kuupongeza uongozi wa TFS kwa usimamizi mzuri wa kuifanya Hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi kuwa ya kipekee na yenye mvuto wa namna yake kwa watalii. "Tumeona uboreshaji wa miundombinu na mazingira ya hifadhi uliofanywa na fedha za Uviko 19, hakika Pugu Kazimzumbwi kunavutia lakini tumieni bajeti binafsi kuendelea kuboresha maeneo yaliosalia," amesema mjumbe wa Bodi CPA. Bahati Lucas Masila.
Naye Wakili Msomi Adv. Piensia Christopher Kiure alisema ameona kazi kubwa iliyofanyika ndani ya hifadhi hiyo na kuwataka Watanzania kumiminika kwa wingi kufahia maisha.
Mathew Ntilicha ni Mhifadhi Mkuu TFS na Kaimu Kamanda wa Kanda ya Mashariki anasema licha ya uboreshaji wa miundombinu, huduma za kiutalii na utangaza wa utalii ikolojia ndani na nje ya nchi kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo TFS bado inaendelea na jitihada za kuhakikisha watalii wanaendelea kuongezeka zinaendelea ikiwemo kuwakaribisha wawekezaji.
“Idadi ya Watalii wa ndani nan je ya nchi inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka, mwaka 2021/2022 tulipokea watalii 18,544 na kukusanya zaidi ya milioni 76 huku idadi ya watalii waliotembelea mwaka huu wa fedha (2022/2023) hadi kufikia mwezi Februari ikiwa ni watalii 16,548 na kukusanya zaidi ya Tshs milioni 100,” anasema Ntilicha.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ni miongoni mwa taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii ziliyopata sehemu ya Shilingi Bilioni 90.2 za Uviko 19 ilizoidhinishiwa Wizara kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli na miradi mbalimbali ya sekta ya utalii na kutekeleza miradi mitano.
Post A Comment: