Jumla ya wananchi 6,500 kutoka mkoani Mbeya wamepatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kununua bidhaa zilizothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) sambamba na kuwahamasisha wafanyabiashara kusajili maduka ya chakula na vipodozi.

Wananchi hao walipatiwa elimu hiyo kupitia kampeni ya kutoa elimu kwa umma iliyoendeshwa na shirika kwenye wilaya hizo ambayo imemalizika mapema wiki hii.

Kampeni hiyo ya elimu kwa umma ilifanyika katika maeneo mbalimbali yakiwemo masoko, stendi, minadani na maeneo mengine ya wazi ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kupata elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali yahusuyo ubora wa bidhaa.

Afisa Masoko wa TBS Deborah Haule, aliwakumbusha wananchi kuwa vita ya bidhaa hafifu sio ya TBS pekee, bali ni ya Taifa kwa ujumla.

"Kampeni hii imeweza kuwafikia zaidi ya wananchi 6,500 kutoka Mbeya mjini na wilaya za Chunya, Busokelo na Mbarali," Alisema Haule.

Haule aliwafafanulia wananchi umuhimu wa viwango katika maisha yao ya kila siku vilevile kuwafahamisha fursa ya huduma bure kwa wajasiriamali wadogo.

Alitaka wawe mabalozi wazuri wa kuhamasisha ubora katika jamii wanazoishi.

Vilevile aliwasisitiza wananchi kuendelea kutoa taarifa pindi wanapokutana na bidhaa zilizokwisha muda wake au wanapotilia shaka bidhaa yoyote katika soko au ziĺizopigwa marufuku kama vile nguo za ndani za mitumba na baadhi ya vipodozi.

Alitoa mwito kwa wafanyabiashara kufuatilia taratibu sahihi za usajili wa bidhaa au majengo kupitia mawasiliano waliyopewa pamoja na kutembelea ofisi ya TBS iliyopo karibu au kupiga katika kituo cha huduma kupitia mawasiliano waliyopewa.

Afisa Tawala mkoa wa Mbeya, Bw. Rodrick Mpogolo aliipongeza TBS kwa kutoa elimu hiyo kwa wananchi katika ngazi ya wilaya, kwani itaongeza ufahamu na kuhakikisha suala la uuzaji wa bidhaa hafifu sokoni linapungua kama sio kwisha kabisa.

Kwa upande wake mjasiriamali mdogo Aristidias Justin kutoka soko la SIDO Mbeya ameishukuru TBS kwa kuwatembelea na kutoa elimu ambapo ameahidi kufanyia kazi elimu waliyopatiwa ili kuzalisha na kuuza bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: