Mjasiriamali Fatuma Abubakar (kushoto) akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya Sh.Milioni 305 kutoka kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu (kulia) zilizotolewa na Halmashauri ya  Manispaa hiyo ikiwa ni mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika hafla iliyofanyika jana, Februari 17, 2023.

..................................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

MSTAHIKI Meya wa Manipaa ya Singida, Yagi Kiaratu amewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kuwa na nidhamu ya fedha na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili iweze kukopeshwa kwa watu wengine.

Kiaratu aliyasema hayo wakati akikabidhi mfano wa hundi ya Sh. Milioni 305 kwa wanufaika hao ambao ni vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambapo vikundi 77 vimenufaika na mkopo huo katika hafla iliyofanyika jana ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida.

Alisema mikopo wanayokopeshwa inatolewa kisheria hivyo wanatakiwa kuitumia katika uzalishaji na si kwa matumizi mengine kama kununua, nguo, chakula na mambo mengine yanayofanana na hayo.

"Tumieni fedha hizi kwa kukuza mitaji yenu na faida mtakayopata kwa ajili ya matumizi yenu sitarajii nije nione mnafikishwa kwenye vyombo vya sheria mkidaiwa fedha hizo kwani ninavyowaona mpo vizuri na mnajitambua na ninyi ni wapambanaji," alisema Kiaratu.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Jeshi Lupembe aliwapongeza wanufaika wa mikopo hiyo ambao wamekuwa wakirejesha kwa wakati na kuwa na sifa tena ya kukopa fedha hizo ambapo alieleza kuwa mikopo hiyo inayotolewa ni sehemu ya asilimia 10 ya mapato ya ndani.

Aidha,Lupembe alisema kwa kipindi cha robo ya tatu 2022/2023 (Januari-Machi), halmashauri ya manispaa hiyo imetenga na kutoa Sh. milioni 305 kwa vikundi vya Wanawake,Vijana na Watu Wenye Ulemavu ambapo kati ya fedha hizo sh. milioni 124  ni asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani ambazo zinatolewa kwa Vikundi 35 (Wanawake 23 Vijana 9 na wenye Ulemavu 3) na sh.  milioni181 ni fedha za marejesho ambazo zinatolewa kwa vikundi 42 (Wanawake 28 Vijana 14 na Walemavu 0.)

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa hiyo, Upendo Naftari  alikitoa taarifa ya mikopo hiyo alisema kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Halmashauri hiyo imetenga bajeti ya Sh. milioni 420 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake,Vijana na Watu wenye ulemavu.

Alisema kwa kipindi cha Julai-Desemba halmashauri imetoa Sh milioni 126 kwa vikundi 32 ambapo kati ya fedha hizo Sh. milioni 80 ni asilimi 10 ya fedha za mapato ya ndani ambazo zilitolewa kwa vikundi 14. (Wanawake 10 Vijana vitatu na Wenye Ulemavu kikundi kimoja) huku Sh. milioni 46 ni fedha za marejesho ambazo zimetolewa kwa vikundi 18 ( Wanawake 12 Vijana vinne na Wenyeulemavu viwili)

"Kati ya fedha zilizokopeshwa jumla ya Sh. 5,300,000 zimerejeshwa na ufuatiliaji wa marejesho unaendelea kwa vikundi vyote vilivyokopeshwa," alisema Naftari.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu akizungumza kwenye hafla hiyo. Mhe.Kiaratu alikuwa mgeni rasmi.
Kaimu Mkurugenziwa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Jeshi Lupembe akizungumza kwenye hafla hiyo.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa hiyo, Upendo Naftari  akitoa taarifa katika hafla hiyo.
Wajasiriamali wakisubiri kukabidhiwa fedha katika hafla hiyo.
Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Hassan Mkata akizungumza kwenye hafla hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala, Kulanga Kanyanga.
Hafla ikiendelea.
Wanufaika wa mkopo huo wakiwa katika piicha ya pamoja na mgeni rasmi.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: