Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, imeandaa mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini unaofahamika kwa Kiingereza "Secondary Education Quality Improvement Program (SEQUIP).



Madhumuni ya mradi huu ni kuongeza ufikiwaji wa elimu ya sekondari, kuwapatia  wasichana mazingira bora ya kujifunza na kuboresha uhitimu bora wa elimu ya sekondari kwa wasichana na wavulana. Unaweza kusoma zaidi juu ya mradi huu hapa

Malengo ya mradi huu ni pamoja na Kuwajengea Wasichana Uwezo Kupitia Elimu ya Sekondari na Stadi za Maisha, Kutoa Msaada wa kitaalamu, Kufanya Tathmini ya Athari ya Mradi na Uratibu wake, Kufundisha na Kujifunza kwa Ufanisi kwa Kuwezesha Mifumo ya Kidigitali na Kupunguza Vikwazo vya Elimu kwa Wasichana  Kupitia Uwezeshaji wa Upatikanaji wa Elimu ya Sekondari Akisoma hotuba yake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na serikali za  mitaa, Mheshimiwa Innocent Bashungwa (MB), akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23 alisema;

“Jumla ya Shilingi bilioni 135.43 zimetengwa kupitia Programu ya Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa shule 10 za sekondari za wasichana za bweni kwa masomo ya sayansi, shule za sekondari 232 za Kata, ujenzi wa shule mpya za kata 184, ujenzi wa shule mpya tano (5) za sekondari za wasichana za bweni kwa masomo ya sayansi na fedha kwa ajili ya ufuatiliaji na tathmini”

Serikali kupitia Ofisi ya Rais Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilitoa miongozo ya ujenzi wa shule hizi katika Halmashauri zote nchinina kuziagiza kukamilisha ujenzi wa shule hizi kabla ya Disemba 2022. Mwongozo huo unapatikana kwenye tovuti ya TAMISEMI hapa.

Moja ya wanufaika wa fedha hizo ni Shule ya Sekondari ya Ayalabe iliyopo Wilayani Karatu. Shule hii ni moja ya shule mpya inayojengwa kwa kutumia fedha za mradi huu maalumu wa SEQUIP.

Halmashauri ya wilaya ya Karatu ilipokea Shilingi Milioni 470 kwa awamu ya kwanza kwa kukamilisha Vyumba vya madarasa 8, Maabara ya sayansi 3, Jengo la utawala, Maktaba, Chumba cha ICT,Vyoo vya wanafunzi 20 (Wavulana 10 na Wasichana 10), Tanki za Maji 2 za lita 10,000, nguzo ya kuwekea Tanki, Ujenzi wa miundombinu ya kunawa mikono sambamba na miundo mbinu ya kuvuna /kuunganisha maji.

Hata hivyo, uchunguzi wetu umeonesha kwamba, mpaka February 2023, Halmashauri hii imeshindwa kukamilisha mradi huu huku fedha zilizotolewa zikiwa zimekwisha. Mbaya zaidi, Mkurugenzi wa Halmasahuri hiyo akitaka kuongezewa kiasi cha fedha kutoka kwenye mapato ya ndani ya halmashauti ili kumalizia baadhi ya majengo ambayo (fedha yake ilitoka SEQUIP) ila bado hayajakamilika.

Kulingana na taarifa kutoka kwa wakazi wa eneo hilo, baadhi ya majengo yameishia kwenye maboma. Ili kujiridhisha, timu yetu iliweka kambi kwenye halmashauri hiyo ili kupata ukweli wa mambo. Shule ya Sekondari Ayabale ipo umbali wa takribani kilomita 140 kutoka Arusha. Tulizungumza na Bi Leah Rashid ambaye ni Mkazi wa kitongoji cha Ayalabe aliyekuwa na haya ya kusema;

"Halmashauri imetoa fedha nyingi katika kujenga misingi ya majengo haya ndio maana mengine unaona yapo hayajakamilika yameishia kwenye maboma wakati yalipaswa kukamilika ,nikweli kulikuwa na mwinuko hapa ila walishindwa nini kusawazisha eneo hili ndipo waanze ujenzi wakaanza ujenzi wa misingi iliyowagharimu."

Maoni ya wakazi wa eneo hilo, yalienda na hali halisi ambayo waandishi wetu waliikuta kwenye shule hiyo na kuchukua ushahidi wa picha zilizoambatanishwa kwenye Makala hii.Ili kupata maelezo kutoka serikalini, tulimtafuta Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu Dr. John Lucian ambaye alikuwa na haya ya kusema juu ya Sakata hilo.

“Ardhi ya pale kwasababu upande mmoja ni mmuinuko imetugarimu sana lakini hakuna pesa zilizoibiwa ni kwasababu pia jengo limejengwa kwa ubora wa hali ya juu kwahiyo kwa kiwango kule tulichopanga kingetosha hakikutosha kwasababu hizo.”

Dr Lucian aliongeza “Jengo lililotumia fedha nyingi ni jengo la utawala na hilo  limekamilika pamoja na madarasa manne lakini hayo yaliyobaki tumekubaliana na   Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi kwamba tutafute fedha kutoka kwa wadau na mapato yetu ya ndani tuweze kukamilisha.”

Hata hivyo, mradi huu sio wa kipekee. Kote nchini, shule zimekuwa zikijengwa kwa kiwango cha fedha kilichotolewa, kwani kama ilivyoelezwa awali, TAMISEMI walitoa mwongozo hadi michoro ya majengo ya shule hizi.

Uchunguzi wetu unaonesha kwamba, baadhi ya halmashauri ambazo zilipokea kiwango sawa cha fedha (milioni 470) zimekua zikichapisha maendeleo ya ujenzi wa shule kwenye tovuti zake. Mfano Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ilichapisha picha za Ujenzi wa shule mpya ya Viziwaziwa kwenye halmashauri ya Mji Kibaha katika kwenye tovuti yake hapa. Shule hiyo nayo ilipelekewa kiasi cha shilingi Milioni 470 kama iliyotengewa Shule ya Sekondari Ayabale.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Kata ya Buzuruga kupitia fedha za  SEQUIP shilingi Milioni 470 ikapatikana shule mpya ya sekondari ya Buzuruga. Halmashauri ilitengeneza hadi video inayoonesha maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo. Je kwanini fedha hizo zitoshe kwenye halmashauri nyingine, na zisitoshe kwa halmashauri ya Karatu?

Kwa upande wake, Bi Leah Rashid alitoa rai hii kwa watendaji wa serikali.

"Niishauri serikali yangu sikivu kuangalia namna gani wanaposhusha hizi fedha huku chini kwa ajili ya maendeleo waje kuzisimamia vyema maana shule hii ilipaswa kukamilika kabla ya Disemba 2022 ila wakaongezewa miezi mingine mitatu sasa inaisha na shule hii ipo vilevile hakuna chochote kinachoendelea, halmashauri ipo nyuma sana kwenye ujenzi huu"

Ikumbukwe serikali ilitoa fedha hizi kwa awamu ya kwanza shilingi milioni 470 ili kukamilisha majengo yote na awamu ya pili mara baada ya kukamilisha ujenzi serikali ingeongezea shilingi milioni 130 kwa ajili ya nyumba za watumishi mbili kwa shilingi milioni 100 na shilingi milioni 30 kwa ajili ya vifaa vya Tehama.



Share To:

Post A Comment: