Serikali ya Korea imeridhishwa na Maendeleo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila na imeahidi kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuwajengea uwezo wataalamu.


Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi Msaidizi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Wizara ya Uchumi na Fedha ya Jamhuri ya Korea Kusini Bw. Young Yoon alipotembelea MNH- Mloganzila ambayo imejengwa kwa ushirikiano na Serikali ya Korea.


“Tumefurahi tumekuta mazingira ya Hospitali ni mazuri, huduma zinatolewa vizuri na takwimu za wagonjwa ni nzuri, tunaahidi tutaendelea kushirikiana” ameeleza Bw. Young


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila Prof. Mohamed Janabi amemueleza Bw. Young kuwa kwa sasa Hospitali ya Mloganzila inaendeshwa chini ya usimamizi wa bodi ya wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili na kwamba inaendeleza majukumu yake ya msingi ambayo ni kutoa huduma za tiba, elimu na utafiti.


“Mloganzila inahudumia wagonjwa wa nje zaidi ya 13,224  kwa mwezi wakati wanaolazwa ni zaidi ya 1245. Hospitali ina watumishi 654, ina jumla ya vitanda 656 kati ya hivyo 12 ni vya kuchuja damu (Dialysis), vitanda 12 vipo vyumba vya upasuaji na vitanda 31 ni kwa ajili ya wagonjwa mahututi (ICU)” alieleza Prof. Janabi


Katika ziara hiyo Bw. Young alitembelea maeneo mbalimbali ya hospitali ambapo aliona na kuridhishwa na hali ya utoaji huduma na kutoa pongezi kwa Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Hospitali.

Share To:

Post A Comment: