Na Angela Msimbira OR- TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki ametoa maagizo saba kwa waganga wakuu wa mikoa na Halmashauri ikiwemo kuwataka kufanya ukaguzi wa vifaa vya afya ili kudhibiti upotevu na matumizi mabaya ya bidhaa hizo.

Aidha, amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri, waganga wakuu na wafawidhi wa vituo vya afya kuhakikisha fedha za Mfuko wa Afya wa pamoja zinatumika kwa wakati na kuzingatia mipango iliyoidhinishwa na hatakuwa na mzaha na watakaokiuka hilo.

Waziri Kairuki alitoa maagizo hayo leo Februari 22, 2023 jijini Dodoma wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa waganga wakuu wa mikoa na Halmashauri ambao uliambatana na uzinduzi wa mwongozo wa utekelezaji wa mshitiri kwenye ununuzi   wa dawa,vitendanishi vifaa na vifaa tiba ili kudhibiti ununuzi holela wa bidhaa hizo.

Waziri  Kairuki amesema kutofanyika kwa ukaguzi wa bidhaa za afya ikiwemo dawa, vitendanishi vifaa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya kunaweza kuchangia upotevu na matumizi mabaya ya bidhaa hizo.

“Nichukue nafasi hii kuwaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuwa kafanyeni ukaguzi wa vifaa vya afya kwa ushirikiano kati ya Idara ya Afya na Wakuu wa Idara nyingine ikiwa ni pamoja na wakaguzi wa ndani.

Pia kuanzia sasa ukaguzi wa bidhaa za afya itakuwa ni moja ya kiashiria cha ufanisi kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri,”alisisitiza Waziri Kairuki.

Amefafanua  kuwa hilo litaenda sambamba na kuhakikusha kuwa vifaa tiba, mashine za maabara na X-ray zilizosambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya, Wahandisi wa vifaa tiba ngazi ya Halmashauri na watumiaji wa vifaa wanajengewa uwezo ili waweze kumudu kuvitumia na kuvifanyia ukarabati au matengenezo Kinga.

Waziri Kairuki amesema kilio cha kuchelewa kwa fedha za mfuko wa afya wa pamoja kimesikika na kwamba kutakuwepo utaratibu wa kutolewa mwanzoni mwa robo mwaka kama ilivyopendekezwa kupitia mkutano huo.

Hata hivyo, kumekuwepo na tatizo la baadhi ya Halmashauri hasa ngazi ya vituo kutotumia fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja hali inayopelekea kuwa na bakaa kubwa, nitumie nafasi hii kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu Mikoa na Halmashauri, Waganga Wafawidhi wa Vituo kuhakikisha fedha hizi zinatumika kwa wakati na kuzingatia Mipango ilioidhishwa

Ameongeza Kwa wale watakaoshindwa kufanya hivyo, tutazihamisha na kuzipeleka kwa wale wenye kuzihitaji zaidi,”.

Mbali hayo amewaagiza wahakikishe  kuwa vituo vyote vilivyokamilika vinaanza kutoa huduma na baadhi ambazo vituo vinakamilika lakini juhudi za kuanza kutoa huduma hazifanyiki na vituo vinafikia hatua ya kuchakaa kabla ya kuanza huduma.

Alieleza katika mwaka wa fedha 2021/ 2022 jumla ya miradi ya miundombinu ya Afya 1,445 ilikuwa inatekelezwa, ikijumuisha miradi ya Zahanati 786, Vituo vya Afya 471 na Hospitali 154.

Aidha, uchambuzi wa utekelezaji wa miradi hiyo unaonesha jumla ya miradi 208 sawa na asilimia 14 ipo katika hatua ya Chini ya lenta, miradi 106 sawa na asilimia 8 ipo katika hatua ya upauaji na miradi 845 sawa na asilimia 58 ipo katika hatua ya umaliziaji.

Amewaelekeza wa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Halmashauri kwenda kusimamia miradi hyoi ikamilike na kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa kwa  wananchi.

Pia, ameagiza kuwa miradi ambayo ipo katika hatua ya upauaji iwe imekamilika ifikapo Februari 28 mwaka huu na miradi iliyo chini ya lenta iwe imekamilika ifikapo Machi 31 mwaka huu

Share To:

Post A Comment: