Na John Walter-Manyara

Vijana wametakiwa kuacha  Uzururaji na kutafuta fursa za ajira ili kukuza uchumi wao, familia zao na Taifa kwa Ujumla.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa chama Cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Peter Toima wakati akifungua semina ya Siku Moja ya Kilimo kwa Vijana wilaya ya Babati yenye lengo la kuwawezesha vijana kufanya Kilimo Biashara ikiwa ni fursa iliyotolewa na serikali nchi nzima ili waweze kujiajiri.

Peter Toima amesema Vijana ni kundi Kubwa hivyo chama Cha Mapinduzi kupitia kwa Mwenyekiti wake Taifa Rais Dr. Samia Suluhu Hassan kimeamua kuja na mpango huo wenye nia ya kuwainua vijana wote kiuchumi na kupunguza wimbi la wategemezi.

Vijana hao wameiomba Serikali mkoa wa Manyara kutenga maeneo kwa ajili ya Shughuli za Kilimo kwa Vijana kwa kuwa maeneo yaliyotajwa kwenye fomu kuhusu mradi huo wa Build Better Tomorrow (BBT)  hayajautaja mkoa huo.

Wamesema  kuwa kwenda kwenye semina katika mikoa mingine ni gharama Kubwa kwani wengine wana familia zao zinawategemea,  hivyo iangaliwe njia rahisi ya kuanzishwa kambi za semina kwenye mkoa ambao vijana wamejitokeza.

Akijibu Swali lililoulizwa na Mohamed Haji,  Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mjini Babati Filbert Mdaki alisema watajadiliana na mkoa kutafuta maeneo kwa ajili hiyo.

Wenyeviti wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) Magdalena Urono wa wilaya ya Babati mjini na Solomon Mpaki wa Vijijini wamesema muamko kwa Vijana ni mkubwa na kwamba wanaendelea kuhamasisha huku wakiwasihi vijana kubadili mtazamo kuwa kilimo ni Kwa ajili ya wazee pekee.

Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange amewataka vijana hao wasikubali kuachia fursa zinapotokea.

Twange amewapongeza Viongozi wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Babati Vijijini na Mjini kwa kujiongeza  kuwaza Jambo la kuwapatia semina vijana ili kuelewa fursa hiyo ya mikopo kwa vijana ambao wapo tayari kujishughulisha na Kilimo.

Aidha Twange amewaambia  vijana wasichoke kuisumbua serikali kupata mikopo isiyo na riba inayotolewa na kila Halmashauri nchini.

Majid Suleiman afisa Kilimo msaidizi Wilaya ya Babati amesema vijana walioamua kujiingiza katika Kilimo ni uamuzi sahihi na kwa wakati sahihi.

Sifa za mwombaji fursa hiyo anatakiwa awe mtanzania mwenye umri kati ya 18-40 na awe anashiriki kwenye Shughuli za Kilimo ambapo muda wa kuomba ni Januari 15,2023 hadi Januari 30,2023, fomu zinapatikana kwenye tovuti ya wizara ya Kilimo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Serikali imetenga Hekari zaidi ya 99 elfu katika mikoa ya  Mbeya, Kigoma,Kagera, Dodoma kwa ajili ya Kilimo kwa vijana.

Share To:

Post A Comment: