Na John Walter-Manyara

Jeshi la Polisi mkoa wa Manyara na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Babati wameungana na wananchi kufanya Usafi katika kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar leo Januari 12,2023.

 

Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara George Katabazi amesema wameamua kuungana na Wananchi kufanya Usafi katika maeneo ya mji wa Babati na Soko kuu kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar pia kuwa karibu na wananchi ili kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwao na kudumisha uhusiano mzuri uliopo.

 

Kamanda Katabazi amesema ili kukomesha vitendo vya uhalifu na ukatili katika jamii, wananchi wanatakiwa kuimarisha ulinzi na kuendelea kutoa taarifa  kwa jeshi la polisi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

 

Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amewapongeza askari wa jeshi la Polisi  na wananchi waliojitokeza kuadhimisha Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kwa kufanya usafi katika eneo la soko kuu Babati.

 

Aidha  Twange ametoa rai kwa wazazi wenye watoto waliohitimu darasa la saba na kufaulu  ambao bado hawajaripoti, kuhakisha wanawapeleka shule watoto wao kwani serikali imejenga madarasa ya kutosha na madawati.

 

Kaimu mkuu wa idara ya Mazingira na Usafi Halmashauri ya mji wa Babati Aretas Laurent amesema wataendelea kushirikiana na wananchi wa mji huo kuhakikisha wanaendelea kupata heshima ya kuongoza kwa usafi nchini na kushika nafasi ya kwanza kama ilivyokuwa mwaka 2022 ambapo walipatiwa cheti na fedha shilingi Milioni 15.

Itakumbukwa kuwa RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi alifuta sherehe za Mapinduzi na  kuelekeza  fedha  zilizotengwa kwa ajili ya Sherehe hizo za Miaka 59 ya Mapinduzi   zitumike katika sekta ya elimu.

Rais Dk Mwinyi alisema sherehe za Mapinduzi mwaka 2023  zilipangwa kutumia Sh milioni 700 licha ya gharama kupunguzwa hadi kufikia Sh milioni 450, ambazo amesema serikali imezielekeza  kuongeza nguvu  kwenye sekta ya elimu ikiwemo madarasa, madawati, maabara na huduma nyingine za elimu.

 

 

Share To:

Post A Comment: