Na Joachim Nyambo.

“UZOEFU unaonesha mara nyingi watoto wachanga wanafariki kutokana na sababu zinazojirudia.Na ukiangalia upatikanaji wa vifaa tiba ni eneo ambalo ni muhimu sana na linaweza likachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya watoto wachanga.”

Ilikuwa miongoni mwa kauli alizozitoa Mratibu kiongozi wa programu ya Nest 360 Tanzania inayotekelezwa nchini na Taasisi ya Afya ya Ifakara,Donat Shamba wakati taasisi hiyo ilipokabidhi msaada wa vifaa   vya kujifunzia masuala ya ukarabati wa vifaatiba kwaajili ya kulinda afya ya watoto wachanga vyenye thamani ya Shilingi milioni 70 kwa chuo kikuu cha Sanyansi na Teknolojia Mbeya(Must).

Kutolewa kwa vifaa hivyo kunalenga kuwezesha upatikanaji wa wataalamu wa matengenezo ya vifaa vinavyotumika kunusuru uhai wa watoto wanaozaliwa ili kuondokana na uhaba wa wataalamu hao uliopo hapa nchini.

Shamba anasema Taasisi imelenga kutoa msaada wa aina hiyo kwenye vituo sita vilivyopangwa kikanda ambapo kwa kanda ya Nyanda za juu Kusini kituo kinachonufaika ni chuo cha Must kilichopo mkoani Mbeya.Vituo vingine ni Arusha,Dodoma,Mwanza kupitia hospitali ya Bugando na Dar es salaam kupitia Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam(DIT) alivyosema vitatumika pia kufundishia wataalamu waliopo katika hospitali za mikoa na wilaya jirani.

Shamba anasema Taasisi hiyo ilichukua uamuzi wa kutoa msaada huo baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto kubwa ya uhaba wa wataalamu wa vifaa vya kulinda maisha ya watoto wanaozaliwa hatua iliyosababisha vifaa vilivyoharibika kutokarabatiwa.

Anasema kutokana na kukosekana kwa wataalamu matukio ya vifo vya watoto wachanga yalionekana kuongezeka katika maeneo mengi hatua aliyosema hailingani na utaalamu uliopo hivi sasa unaoweza kuwaokoa kwa kiasi kikubwa watoto hao wachanga na kuwafanya waishi.

“Matatizo ya afya ya watoto wachanga mengi ni mtambuka na yanahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kupata ufumbuzi.Ndiyo sababu tukaamua kushirikiana na Taasisi kama Must ili kutoa sehemu ya suluhu kwa kuwapika wataalamu watakaokuwa msaada wa kukarabati au kutengeneza vifaa tiba vinavyotumika kuokoa maisha ya watoto wachanga pale vitakapoharibika.”

“Kama programu ya Nest Tanzania kuwa na Byomedicaskills lab nyingi  nchini lakini kwa kuanza tumeanza kwa kushirikiana na chuo cha Must hapa na uongozi wa afya wa mkoa hapa itaweza kusaidia Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na mikoa jirani.”

“Tunatarajia ujuzi ambao wataalamu hapa wanaupata wa namna ya kuvitumia na kufanyia matengenezo itasaidia sana uharaka katika vituo vinavyotoa huduma  na hatimaye watoto watapata huduma inayostahili kwa haraka sana.”

Shamba anasema matarajio ya program hiyo ni kuona ujuzi wa matengenezo wa vifaa hivyo unaenea kwa kasi kupitia wataalamu kuambukizana kile wanachojifunza katika karakana iliyopewa uwezo wa vifaa iliyopo Must.

“Wataalamu wa hapa watakwenda kuwafundisha wauguzi,madaktari,wakunga na wote wanaofanya kazi katika vituo hususani wanaotoa huduma ya mtoto.Tunatarajia vitaleta mabadiliko makubwa sana.”

“Kama mnavyojua kwamba mipango ya milenia ni kwamba ifikapo mwaka 2030 kuwe na vifo chini ya 12 hivyo tukiweka juhudi hizi tukishirikiana na serikali  tunaamini tutafika huko kama kila kitu kitafanyika vile inavyostahili.”

Anafafanua kuwa Programu ya Nest inayaangalia maeneo makuu matatu ambayo ni vifaa,utaalamu na kwa kushirikiana na serikali kushauriana kuona namna ya kuboresha mitaala vyuoni ili iendane na mahitaji ya sasa sambamba na  namna bora ya ukusanyaji takwimu za watoto wachanga.

“Tumekuwa na programu mbalimbali za kuwajengea uwezo watoa huduma yaani manesi na madaktari.Lakini pia tumekuwa tukishirikiana na wizara kuangalia namna gani tunaweza tukabadilisha au kuboresha mitaala iliyopo kwa sababu kwa sasa hapa Tanzania hakuna chuo kinachofundisha Neonato Nurses tuna neto meadwife.”

“Inabidi tuwe na watoa huduma kwa watoto wachanga zaidi kwa sababu ni kundi gumu kwa maana kuwahudumia inahitaji utaalamu mahususi.Pia tumekuwa tukishirikiana na wizara kuboresha ukusanyaji wa takwimu za watoto wachanga.Sasa hivi hakuna Register ya watoto wachanga sasa tuko katika mpango wa kuitengeneza ili  taarifa zote zinazohusu watoto hawa zikusanywe kwa usahihi ili ziweze kusaidia watoa huduma kufanya maamuzi sahihi.”

“Hauwezi kufanya maamuzi kama hauna taarifa hivyo upatikanaji wa taarifa sahihi tunadhani utasaidia sana kufanya maamuzi sahihi kwenye utoaji wa huduma na hata maamuzi mengine.Hapa tumesema ifikapo 2030 tuwe na vifo chini ya 12 lakini bila kuwa na takwimu hatuwezi  kujua watoto wangapi tumewahudumia ,wangapi hatujawahudumia au wangapi tumewahudumia wakapata shida gani.”

Anasema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na,Tamisemi wanayo imani yakupunuza vifo vya watoto wachanga kwa asilimia kubwa na ikiwezekana kuvifuta kabisa kwakuwa malengo ni kila mtoto anayezaliwa aishi.

Elizabeth Ngowi ni mhandisi wa vifaa tiba wa programu ya Nest 360 Tanzania.Alivitaja vifaa vilivyotolewa kwa chuo cha Must kuwa ni pamoja na mashine ya kutibu watoto wachanga waliozaliwa  na tatizo la manjano ya ngozi na mashine ya joto kwa watoto wachanga.

Nyingine ni mashine ya kusaidia kufungua mapafu ya mtoto mchanga ili aweze kupumua vizuri,mashine ya oksijeni inayomwezesha mgonjwa kupata  hewa ya kutosha,mashine ya kutoa vitu visivyotakiwa katika mwili wa mtoto anapozaliwa na mashine ya kuangalia kiwango cha oksijeni kinachoingia mwilini iwapo kinatosha.

 

Zipo pia mashine ya kuangalia kiwango cha sukari cha sukari katika mwili wa mtoto na pia zana kutengenezea mashine hizo ambapo vifaa vyote hivyo vitatumika katika kuwafundishia wanafunzi waliopo chuoni hapo wanaosoma masomo yanayohusiana na utaalamu wa vifaa tiba.

Katika kuleta tija zaidi,Ngowi anashauri zana hizo pia zitumike kuwafundishia wataalamu waliopo tayari kazini kupitia programu mbalimbali zinazoweza kuandaliwa ili kupunguza kwa haraka changamoto ya wataalamu wa vitendea kazi hivyo alivyosema ni muhimu katika kuokoa maisha ya watoto.

Naibu Makamu mkuu wa Chuo cha Must,Profesa Godliving Mtui anasema msaada huo utakuwa chachu ya kuzalisha kwa wingi wataalamu watakaokwenda kusaidia maisha ya watoto wachanga na kuwaepusha na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Profesa Mtui pia alisisitiza umuhimu wa wadau wa sekta ya afya kutambua umuhimu wa wataalamu wa matengenezo ya vifaa tiba na kuandaa utaratibu wa utoaji ajira akisema tayari chuo hicho kimeanza kuzalisha wataalamu lakini wanapohitimu upatikanaji wa ajira zao bado ni mgumu.

Anasema hali hiyo inatokana na wadau wengi kutotambua uwepo wa wataalamu hao na hivyo kubaki wakikabiliwa na changamoto ya kushindwa kutoa huduma kutokana na kuwa na vitendea kazi vibovu na kubaki wakisubiri wataalamu watoke nje ya nchi kuja kuwasaidia.

 

“Tunazo programu ambazo tunazitoa moja ikiwa ni ya Stashahada ya vifaatiba na uhandisi wake..lakini tunashirikiana na Taasisi ya Chuo Kikuu cha Sayansi cha Tiba na Sayansi  zinazohusiana na Tiba cha Muhimbili yaani MUHAS kutoa Shahada ya vifaa tiba.”

“Kama Taasisi ya elimu ya juu tumefurahi sana kupata vifaa hivi…vitatusaidia sana kuongeza ubora na tutahuwisha mitaala yetu ili tuweze kuboresha mafunzo yanayotolewa hapa na mafunzo yanayotolewa hapa tunayaita Elimu ujuzi.Wanapotoka wahandisi wetu hapa na mafundi mchundo wanakuwa tayari wana ujuzi kabisa wa kwenda kufanya kazi.Hata katika hili tutatoa wahitimu walio mahiri sana ili wakasaidie taifa letu kupiga hatua kimaendeleo.”

Magdalena Manjano ni mratubu wa Huduma za Afya ya uzazi Mkoa wa Mbeya.Akimwakilisha mganga mkuu wa mkoa katika hfla ya kupokea vifaa hivyo anapongeza Taasisi ya Ifakara kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kupunguza  vifo vya vitokanavyo na uzazi na mtoto.

“Sote tunajua vifo vya uzazi na mtoto kwa sasa vinapigiwa kelele ili vipungue katika nchi yetu.Vifo vya uzazi na mtoto mara nyingi vinatokea kwa ghafla mno kiasi kwamba kama hatuna vifaa tiba,kama hatuna wataalamu wa kutosha wa kuzuia katika ngazi ya chini kwqenye jamii mpaka kwenye vituo tunaweza kuwapoteza wajawazito na watoto wachanga kwa muda mfupi sana.”

“Katika kipengele cha vifo vya watoto,walio wengi wanafariki ndani ya siku saba na mashine au vifaa tiba pekee ndivyo vinaweza kuwaokoa watoto wetu katika matibabu yao.Matibabu mengi ya watoto wachanga yanategemea zaidi vifaa tiba.”

Ushirikiano huu wa wadau yaani Taasisi ya Ifakara,Must na Wizara ya Afya wenye kuonesha nia ya kuokoa maisha ya watoto wachanga kwa kuanza kuzalisha wataalamu wa matengenezo ya vifaatiba ni njia muhimu sana.Hii inakwenda sambamba na juhudi zinazofanywa na serikali za kuhakikisha watoto wanaozaliwa wanakuwa katika mikono salama na sahihi.

Share To:

Post A Comment: