
Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Bi.Charty Sichona, ametoa wito kwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa njia ya kidijitali kupitia Benki ya CRDB, kuhakikisha wanatumia fedha hizo kikamilifu katika kuendeleza miradi yao ya kiuchumi ili kufikia malengo ya kujikwamua kiuchumi na kuinua maisha ya jamii kwa ujumla.
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya kutoa elimu ya fedha kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu walionufaika na mikopo hiyo, Bi. Sichona alisema kuwa mikopo hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya taifa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, hivyo ni lazima itumike kwa umakini na uadilifu.
“Natoa rai kwa wanufaika wote wa mikopo hii kutumia fedha hizo kama ilivyokusudiwa. Mikopo hii si kwa matumizi binafsi, bali kwa kuendeleza miradi ya uzalishaji ili kuongeza kipato na hatimaye kurejesha mkopo huo kwa wakati,” alisema Bi. Mlelwa.
Aidha, aliwataka wanufaika kuendelea kushirikiana na maafisa maendeleo ya jamii waliopo katika kata zao kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu juu ya usimamizi wa fedha na uendeshaji wa miradi ili mikopo hiyo iweze kuwa na matokeo chanya ya muda mrefu.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa CRDB Foundation, Fadhiri Bushagoma, ametoa wito kwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa makundi maalum kupitia Benki ya CRDB, kuwa na nidhamu ya fedha ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta tija na kufanikisha malengo ya kiuchumi ya wanufaika.
Aliongeza kuwa lengo kuu la mikopo hiyo ni kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji, hivyo ni muhimu kwa kila mnufaika kuwa na mpango mzuri wa matumizi ya fedha, ufuatiliaji wa mapato na marejesho kwa wakati.
Kwa upande wao, baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo waliishukuru CRDB na Halmashauri ya Jiji kwa kuweka mazingira rafiki ya kupata mikopo, wakisema kuwa sasa wameweza kuanzisha miradi ya ufugaji, kilimo cha mbogamboga na biashara ndogondogo zinazowapa kipato cha uhakika.
Mpango wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri hutolewa kwa makundi maalum kwa mujibu wa sheria ya Serikali za Mitaa na kusimamiwa kwa karibu na idara ya maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na taasisi za kifedha kama CRDB.



Post A Comment: