Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) linaunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utunzaji wa mazingira. Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti, kwa niaba ya Katibu Mtendaji, Mhandisi Enock Kayani ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Mitaala amesema NACTVET inaunga mkono jitihadi za utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti - hususani kwenye maeneo ya shule mbalimbali za msingi na sekondari ili kuwajengea uelewa wa kujali mazingira vijana wadogo ambao ndio taifa la kesho. “Vilevile, kufanya hivi ni kuweka alama inayoishi kwa vijana hawa ili waendeleze utamaduni wa kupanda miti kwa vizazi vijavyo katika kuenzi na kutunza mazingira”. Amesema Mhandisi Kayani.

Mhandisi Kayani amesema kuwa NACTVET itaendelea na zoezi hili kwenye shule zetu kwa kuwashirikisha wanafunzi hao na kuwapa nafasi ya kupanda miti shuleni na kukabidhiwa kuitunza ili ije iwasaidie baadae kwa kivuli  na kupata hewa safi katika mazingira yao kipindi wawapo shuleni. “Zoezi hili ni endelevu kwani linatekeleza agizo la Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo ambayo amekuwa akiyatoa ya kuhakikisha ajenda ya mazingira inatekelezwa kikamilifu na kuifafanua kuwa ajenda hiyo itakuwa ya kudumu”. Amesema

Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania NACTVET inatoa wito kwa wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla kuona umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kuwajengea uwelewa vijana wadogo ambao ni taifa la kesho. Mfano huu ni wa kuigwa na Watanzania wote kwani Mazingira ni uhai na yanamgusa kila binadamu katika nyanja zote za maisha ya kila siku.

NACTVET imefanya zoezi hili la upandaji miti katika Shule ya Msingi Mapambano, iliyoko Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Januari, 2023 katika maeneo yaliyo wazi kwenye shule hiyo kwa kushirikiana na Kaimu Afisa Elimu Manispaa ya Kinondoni Bi. Martha J. Kussaga, Mkuu wa Shule ya Msingi Mapambano Bi. Gwamaka Mwakyusa pamoja na Wanafunzi

Share To:

Post A Comment: