Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amewataka Wataalam wa Mipango miji kutambua kuwa zoezi la utwaaji Ardhi ni la ushirikishwaji tofauti na baadhi ya wataalam wanavyofanya bila kushirikisha Wananchi.


Naibu Waziri ameongeza kuwa vitendo hivi havikubaliki na kuitaka bodi ya wataalam wa mipango miji kutoa elimu kwa wataalam hao kuacha tabia hiyo inayochangia kuleta migogoro mikubwa kwa wananchi hususani katika maeneo ya miji ambapo miradi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi imekuwa ikiendelea.

Naibu Waziri Kikwete amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya usajili wa wataalam wa Mipango miji na kuonya kuwa ni vibaya sana kwa wataalam hao kukiuka taratibu za kitaaluma suala linalopekea wanasiasa kungilia kati ili kutoa maamuzi ambayo kwayo pia yanaweza kuchochea migogoro kwani wanasiasa sio wataalam wa fani hiyo.

Ridhiwani Kikwete ameonya tabia ya kutosimamia mipango miji waliyoiweka inasababisha miji kuvurugwa kwani kwasasa kila mahali kuna ujenzi wa vyumba vya maduka au vituo vya mafuta na baa katika makazi ya watu.

‘’Haya ni mambo ambayo Bodi inapaswa kuyasimamia kwani uzinduzi wa Bodi hii ni suala muhimu sana katika mustakabali wa ukuaji wa taaluma ya Mipangomiji, kwani Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya Bodi ndizo pande mbili ambazo zinaungana pamoja katika kuikuza na kuisimamia taaluma ya mipangomiji nchini’’. Aliongeza Ridhiwani Kikwete.

Kikwete ameitaka bodi hiyo kuzingatia uzoefu na weledi wajumbe wa Bodi hiyo walionao katika fani mbalimbali, kushirikiana kikamilifu na Wizara kuendeleza taaluma ya Mipangomiji kwa pamoja na kufikia lengo la kusimamia Wataalam wa Mipangomiji na kampuni za upangaji miji.

‘’Usimamizi wenu utafanya Wataalam na Kampuni za Mipangomiji zifanye kazi kwa weledi na kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za upangaji miji, kutoa huduma bora, kuweka mazingira ya kuvutia Wataalam wa Mipangomji waliokidhi vigezo vya kusajiliwa ili wasajiliwe, pia kuzalisha fursa zaidi za ajira na kuongeza mchango katika pato la Taifa.’’Aliongeza Ridhiwani Kikwete Naibu Waziri wa Ardhi.

Naibu Waziri Ridhiwani Kikwete alisema Sekta ya Ardhi ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa na kwa kila mwananchi akiongeza kuwa Ardhi ni msingi wa kipekee wa maendeleo na ni rasilimali isiyoongezeka.

Naibu Waziri Kikwete ameiambia bodi hiyo kuwa suala la kupanga ardhi kwa nchi nzima, mijini na vijijini linatokana na ukweli kwamba rasilimali ardhi haiongezeki wakati idadi ya watu na shughuli zao zinaongezeka.

Akitolea mfano wa Nchi yetu Naibu Waziri Kikwete alisema Tanzania ina eneo lenye ukubwa wa takribani kilometa za mraba 948,132.89, ikijumuisha kilometa za mraba 62,032.89 za maji uku eneo la nchi kavu lina ukubwa wa kilometa za mraba 886,100, ambapo Tanzania bara ni kilometa za mraba 883,600, na Zanzibar ni kilometa za mraba 2,500.

Aidha Naibu Waziri huyo wa Ardhi aliongeza kuwa kuna ongezeko la watu kutoka watu 43,625,354 Sensa ya watu 2012, hadi kufikia watu 61,741,120 Sensa ya Watu na Makazi 2022 wakati idadi ya watu ikiongezeka, ukubwa wa ardhi bado ni uleule.

Kikwete aliongeza kuwa kwa kuzingatia ukweli huo, Wataalam wetu pamoja na kampuni za upangaji miji ni muhimu ziendelee kupanga ardhi kwa weledi wa hali ya juu kwani ikifanyika vinginevyo, tutashuhudia ongezeko la migogoro ya ardhi baina ya watumiaji mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji, wachimbaji madini na hifadhi za Taifa.

Kwa upande wa mijini Naibu Waziri huyo alisema, matokeo yake yamejidhihirisha kupitia ongezeko la uendelezaji wa miji isiyopangwa na ukuaji wa makazi holela na kuitaka bodi kufanyia kazi changamoto hizi ili zitatuliwe kwa kupanga ardhi mijini na vijijini ili uendelezaji miji ufuate mipango ya matumizi ya ardhi.

Aidha, Naibu Waziri Kikwete ameitaka bodi pamoja na wataalam wa Mipango Miji kubuni mbinu za namna bora ya kuimarisha utendaji kazi wa Wataalam na Kampuni za Upangaji Miji pamoja na kuibua mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili taaluma ya mipangomiji na Sekta ya Ardhi kwa ujumla, hasa utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Ridhiwani Kikwete aliongeza kuwa ushirikishaji wa wadau wote katika upangaji wa Ardhi ni suala la msingi ili kuepusha migogoro pamoja na hasara za kiuchumi na kimazingira, ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mipango hiyo.

Naye Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo Prof. John Lupala akitoa mwelekeo wa bodi yake alisema Bodi yake kwa mwaka wa fedha ujao itaanzisha mfumo wa kufuatilia wataalamu wa mipangi miji ili kuweza kuwafuatilia kwa akaribu ili kuwazawadia wanaofanya vizuri na kutoa adhabu kwa awale wanaokiuka taratibu.

Prof. Lupala aliongeza kuwa Mfumo huu pia utawezesha bodi kuona kwa karibu kinachoondelea kwa wataalamu wa mipango miji lakini pia kuhakikisha wanaanza taratibu za usajili kwa wataalamu wa wapya kuanzia taratibu za awali mpaka usahili kwa wataalami hao.
Share To:

Post A Comment: