Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iramba mkoani Singida, Augustino Matomola na wenzake sita wamefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakituhumiwa kwa uhujumu uchumi na matumizi mabaya ya ofisi.

Watuhumiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo jana Ijumaa Januari 13 mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi, Edmund Kente na kusomewa mashitaka hayo wanayodaiwa kuyatenda wakiwa watumishi wa Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama na kusababisha hasara ya Sh138 milioni.

Akisoma mashitaka hayo, wakili wa Serikali Satuninus Kamala amesema washitakiwa katika kesi hiyo namba 1/2023 walitenda kosa hilo mnamo Mei 14, 2019.

Mbali na Matomola, wakili Kamala amewataja watuhumiwa wengine ni pamoja na Sungwa Mkenya ambaye ni mhandisi wa majengo katika halmashauri hiyo ya Ushetu pamoja na aliyekuwa mganga mkuu, Nicodemas Sengeo na Shile Ndegeleke ambaye alikuwa Mhasibu.

Wengine Pastory Kayaga (mhasibu), Frank Gondwe na Hussein Kijanga (fundi seremala), ambao wakili huyo wa serikali aliiambia mahakama hiyo wanakabiliwa na makosa saba na upelelezi wake umekamilika.

Wakili Kamala ameiambia mahakama hiyo mshitakiwa namba moja (Matomola), anakabiliwa na makosa manne, ikiwa ni pamoja na kutumia mamlaka aliyokuwanayo kusaini mikataba ya ujenzi wa milango na madirisha 197 ya hospitali ya Halmashauri ya Ushetu bila kuishirikisha bodi ya zabuni.

Kosa la pili kwa mkurugenzi huyo ni kushindwa kushindanisha zabuni ya utengenezaji wa milango na madirisha 197 ya Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu na kumfanya Hussein Kijanga kupata mkataba wa Sh138 milioni kwa ajili ya ujenzi wa milango na madirisha hayo gharama ya Sh700,000 mlango mmoja.

Amesema kosa la tatu kwa mkurugenzi huyo ni kuvunja sheria ya ununuzi namba 167 (1) GN namba 446 ya mwaka 2013 kwa kushindwa kutafsiri masharti ya kiasi cha malipo ya ujenzi ya milango na madirisha 197. 2019 kupitia kwa mkurugenzi, mweka hazina, mganga mkuu na mhasibu msaidizi na fundi selemala waliisababishia halmashauri hiyo hasara ya Sh30 milioni.

Kosa lingine linalowakabili Sungwa Mkenya, Nicodemus Sengeo, Shile Ndegeleke, Frank Gondwe pamoja na Pastory Kayaga wote kwa pamoja wanadaiwa kati ya Mei 14, 2019 hadi Juni 20, 2019 walimficha mkurugenzi wao kwa Kijanga kwa kulaghai na kusaidia kutenda kosa.

Washitakiwa wote wamepelekwa gerezani baada ya kushindwa kukidhi vigezo vya dhamana ambao kesi hiyo itatajwa tena Januari 17, 2023 katika mahakama hiyo na mshitakiwa namba 5, Nicodemus Sengeo ataunganishwa na wenzake baada ya kukamatwa juzi jioni.


H T : Mwananchi

Share To:

Post A Comment: