Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewafikisha mahakamani Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Ruben Mfune na Katibu Tawala Msaidizi wa Fedha mkoani Kilimanjaro, Juma Masatu kwa tuhuma za uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh51 milioni.

Wawili hao walidaiwa kufanya makosa hayo walipokuwa watumishi wa halmashauri ya Ruangwa mkoani Lindi kati ya mwaka 2012 hadi 2015.

Kesi hiyo ilitajwa juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mariam Mchumba.

Katika kipindi hicho, Mfune alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Ruangwa kuanzia 2012 hadi 2015, huku Masatu alikuwa Mweka Hazina wa halmashauri hiyo kwa mwaka 2014.

Halmashauri hiyo katika kipindi hicho, ilipokea fedha kutoka hazina Sh200 milioni kwa ajili ya uchimbaji visima 11 kwenye vijiji vilivyokuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji.

Zabuni ilitangazwa na kupatikana mzabuni atakayechimba visima hivyo kwa Sh182 milioni, lakini baada ya muda wawili hao walidaiwa kuchukua Sh192 milioni na kufanya matumizi mengine kisha wakavunja mkataba na mzabuni.

Hatua hiyo ilimsababisha mzabuni kuishitaki halmashauri na kudai fidia ya Sh200.4 milioni.

Hata hivyo, washitakiwa hao walimaliza kesi hiyo nje ya mahakama kinyume na utaratibu na hivyo kuisababishia Serikali hasara ya Sh51 milioni.

Hata hivyo, haijabainishwa iwapo Sh200.4 milioni za fidia kwa mzabuni zililipwa ama la.

Watuhumiwa walikana tuhuma hizo na shauri litasikilizwa tena Februari 7, mwaka huu huku upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Peter Camilius ulidai upelelezi umekamilika na utawasilisha mashahidi wanane na vielelezo sita.

Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Siyangoi haujasema chochote mbele ya mahakama na watuhumiwa wameachiwa kwa dhamana.


H T : Mwananchi

Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: