Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imetembelea mradi wa maji wa Mugango, Kiabakari, Butiama na kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi huo.

Mradi huo unatekelezwa katika chanzo cha maji ya ziwa victoria eneo la Mugango na utagharimu takribani  shilingi Bilioni 70.5 ambapo utahudumia zaidi ya vijiji 39 vya Halmashauri za Wilaya ya Butiama na Musoma.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo Makamu Mwenyekiti wa Kamati  hiyo, Mhe. Almas Maige (Mb) amesema mradi huo umetekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na kuitaka Wizara ihakikishe inasimamia ili ukamilike haraka.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasan  kwa kuonesha nia ya dhati ya kuondoa adha  ya huduma ya maji kwa watanzania.

Amesema Wizara itahakikisha inasimamia ili kuhakikisha dhamira ya njema ya Rais ya kumtua mama ndoo kichwani inafanikiwa huku Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mhe. Sospeter Mhongo akiwataka wananchi wa Musoma Vijijini kuiamini serikali kwani mradi huo utavifikia vijiji vyote vinavyopitiwa na mradi.


Share To:

Post A Comment: