Mkazi wa Sanawari, Wilaya ya Arumeru Mkoa Arusha, Nelson Mollel (32) amefariki dunia baada ya kudaiwa kupewa adhabu ya kuchapwa vikobo 280 kutokana na tuhuma ya kumtukana mama yake mzazi.

Wazee wa jamii ya Kimaasai na Kimeru wilayani Arumeru mkoani Arusha wamekuwa wakitoa adhabu ya kuwachapa viboko vijana ambao wamekuwa wakibainika kufanya matendo ambayo ni kinyume cha maadili.

Miongoni mwa matendo hayo ni pamoja na kutukana wazazi, kunywa pombe mchana na kufanya vurugu, kuvaa nguo ambazo sio za heshma na kufanya uhalifu ikiwepo kupigana.

Mama mzazi wa marehemu Nelson, Janeth Kimario amesema kijana wake alimtukana Matusi ya nguoni Januari 1, 2023.

Amesema baada ya kutukwanwa ndipo alimwambia baba yake mdogo, Abel Mboya (45) ambaye alifanikiwa kumpata Nelson na kumpeleka porini na kuanza kumchapa fimbo akiwa na watu wengine.

“Lakini adhabu ilikuwa kubwa sana na kweli alistaili kuchapwa ila wamezidisha hadi nimempoteza mwanangu," amesema

Dada wa marehemu, Jackline Elias Mollel amesema mdogo wake amepigwa viboko 280 badala ya fimbo 70 vinavyopaswa kwa mujibu wa taratibu zao.

"Hii ni mila na desturi zetu, sisi Wamasai lakini wamezidisha na pia wamemchapa kwa sifa sana, wamemvunja mbavu miguu na mikono," amesema

Polisi Wilaya ya Arumeru wamethibitisha kupokea taarifa hizo hata hivyo, afisa mmoja wa polisi katika wilaya hiyo jina linahifadhiwa amesema msemaji ni Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha.

"Wewe unajua utaratibu, msemaji ni kamanda na nadhani mkimfuata atawapa taarifa rasmi ni kweli tukio hilo limeripotiwa,"amesema

Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha, Justine Masejo alipotafutwa kwa simu kuelezea mauaji hayo hakupatikana kutokana na simu yake kutopokelewa.

Share To:

Post A Comment: