Na Elizabeth Joseph,Monduli.


KATIKA kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana Serikali Wilayani Monduli imeelekeza Shule zote za Msingi na Sekondari kuwa na utaratibu wa Walimu na Wazazi ama Walezi kusaini pindi wanapowachukua watoto wao shuleni pamoja na kuwa na Walimu wa jinsia tofauti kwenye magari ya Shule.


Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Monduli Bw,Robert Siyantemi wakati akiongea na Waandishi wa Habari juu ya mikakati ya kupunguza Vitendo vya Ukatili wilayani humo.


Ameeleza kuwa ni kuwepo na mahali pa kusaini wakati mwanafunzi anapotoka Shule kurudi nyumbani itasaidia kupunguza vitendo vya Ukatili kwa kundi hilo ikiwa ni pamoja na kila mmoja kuwa makini katika uangalizi wa watoto hao.


"Watoto wote wakike na wa kiume wanapoondoka kwenye Shule zao kuwe na utaratibu wa kusaini wameruhusu watoto wangapi na Wazazi pia wasaini kupokea watoto wao hii itasaidia kuongeza Ulinzi na Usalama wa watoto wetu"amesema Siyantemi.


Aidha aliwaomba vijana nchini kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kuwalinda watoto wakike na wakiume dhidi ya vitendo hivyo jambo alilosema kufanya hivyo kutasaidia kuimarisha ulinzi na kutengeneza taifa Bora kwa baadaye.


"Kuna usemi unasema mchelea mwana hulia mwenyewe,wapo mawakala wanaeneza vitendo vya ushoga,kusagana hawa ni maadui na mawakala wanaolenga kuangamiza vizazi vyetu na taifa la baadaye,tupinge mmomonyoko wa maadili katika jamii zetu na kuwalinda wadogo zetu"alibainisha Katibu Tawala huyo.


Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi ya Monduli Valley Bw,Lothi Leonard aliipongeza serikali ya Wilaya hiyo kwa maelekezo hayo na kusema wako tayari kutatekeleza ili kuwalinda watoto Shuleni.


Mwalimu Leonard pia aliwaomba wazazi na walezi kuhakikisha wanajenga mahusiano rafiki na yenye uwazi kwa watoto wao ili kumsaidia mtoto kueleza changamoto yeyote anayokutana nayo katika ukuaji wake ndani ya Jamii inayomzunguka.


"Wazazi na Walezi wengi wao jukumu la malezi wametuachia Walimu wao wamekuwa bize kutafuta hela na kusahau jukumu lao malezi hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa mtoto kuharibika kitabia bila wao kujua"alisisitiza Mwalimu Leonard.


Mwisho.

Share To:

Post A Comment: