Joto la mama wakati mtoto anapokuwa akinyonyeshwa husababisha uhusiano mwema kati ya wawili hao.

Na Abby Nkungu, Singida

IMEFAHAMIKA kuwa asilimia 42.3 ya watoto wachanga mkoani Singida hawanyonyeshwi  maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya kwanza tangu kuzaliwa kinyume na ushauri wa wataalamu hali inayoathiri maendeleo ya afya, malezi,  makuzi na usalama wa kundi hilo.

Hayo yalibainishwa katika taarifa ya utafiti wa Kitaifa kuhusu lishe mkoani Singida kwa mwaka 2018 (TNNS 2018) inayoeleza hali ya udumavu, ukondefu na uzito pungufu kwa watoto.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 57.7 ya watoto wachanga ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza kama inavyoshauriwa na waatalamu  wa afya  huku  asilimia 42.3 wakichanganyiwa na vyakula vingine.

Mbali na suala la unyonyeshaji, utafiti  huo pia unaonesha kuwa asilimia 29.8 ya watoto walio chini ya miaka mitano mkoani Singida wana udumavu, asilimia 5 wana ukondefu na asilimia 15 wana uzito pungufu.

Daktari Nkosiyabo Masuku wa Taasisi ya Pride Women's Clinic ya mjini Singida anasema kuwa mtoto hapaswi kupewa chakula kingine chochote wala maji ya kunywa kwa kipindi chote cha miezi sita ya kwanza tangu kuzaliwa badala yake anyonyeshwe maziwa ya mama pekee.

Dk Masuku anafafanua kuwa hii ni kutokana na ukweli kwamba utumbo wa mtoto unakuwa bado laini na hauwezi kupitisha vizuri vyakula vingine zaidi ya maziwa ya mama na umeng'enyaji wa vyakula vingine unakuwa mashakani; hivyo kuweza kumuathiri mtoto huyo kiafya.

 "Kwa kweli, maziwa ya mama ni kila kitu. Ni chakula chenye lishe ya kutosha kwa mtoto kwa kipindi hicho lakini pia ni maji. Maziwa ya mama yanaendana na ukuaji wake" alieleza Dk Masuku.

 Alionya juu ya tabia ya baadhi ya akinamama wanaokamua maziwa yao na kuyahifadhi kwenye chombo ili mtoto wake apewe wakati yeye yupo kwenye majukumu mengine akisema kuwa maziwa hayo hupoteza ladha yake halisi ikilinganishwa na yale mtoto anayopata moja kwa moja kutoka kwa mama yake.

"Kadhalika, kitendo hicho kinaondoa ukaribu wa mama na mtoto kwa mtoto kukosa joto la mama na uhusiano wa ana kwa ana baina ya mama na mtoto wakati akinyonya. Mtoto anapokuwa akinyonya hufurahia kuona sura ya mama yake na huhitaji mama naye amwangalie. Hiyo hudumisha uhusiano mzuri baina yao” alifafanua.

Alisema kuwa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto iliyoanza kutekelezwa Januari mwaka 2021 hadi mwaka 2026, inaweza kuwa mwarobaini wa kuhakikisha kila mdau anatimiza vyema wajibu wake na kuleta matokeo chanya katika jamii.

Alisema, kwa kuwa chini ya Programu hiyo wadau wanashughulika na masuala yote mtambuka kwa watoto walio chini ya miaka minane ikiwemo afya, lishe, elimu na ulinzi ni dhahiri suala la elimu juu ya umuhimu wa unyonyeshaji maziwa ya mama pekee kwa miezi sita litapewa kipaumbele.

Hata hivyo, baadhi ya akinamama wanasema kuwa mfumo wa maisha na changamoto zake ni miongoni mwa sababu za watoto kutonyonyeshwa miezi sita mfululizo bila kuchanganyiwa  na chakula kingine.

“Sawa kitaalamu inashauriwa hivyo ila hebu fikiria sisi Ma-Single mother ukae unanyonyesha mtoto muda wote huo wakati unatakiwa uende ukatafute riziki ya watoto wengine kwani sio kwamba una mtoto mmoja tu”  alisema Amina Almasi, mkazi wa  Utemini Singida mjini.

Kwa upande wao, Sauda Ali na Sara Mpinga wote wakazi wa Unyankindi Singida wanasema pamoja na changamoto za kimaisha njia pekee ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa unyonyeshaji maziwa ya mama pekee kwa miezi sita mfululizo ili kujiepusha na athari zinazoweza kujitokeza kwa kuacha kufanya hivyo. 

Mtoto akifurahia ziwa la mama yake katika umri anaopaswa kuwa karibu na mama.
Unyonyeshaji maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya kwanza bila kumuongezea chakula kingine ni muhimu kwa afya ya mtoto kama afanyavyo mama huyu mwenye watoto mapacha. 


Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: