MAGONJWA Yasiyoambukiza kama ugonjwa wa moyo,saratani na kisukari,yanatajwa kuchangia asilimia 71 ya vifo duniani kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) huku visababishi vikuu vikitajwa kuwa ni kutofanya mazoezi,kutopata usingizi wa kutosha na ulaji wa vyakula usiofaa.


Pia WHO inakadiria kuwa kutoshughulisha mwili kunachangia asilimia 6 ya vifo vyote duniani,asilimia 17 ya magonjwa ya moyo na kisukari,asilimia 12 kuanguka kwa wazee na aslimia 10 ya saratani za matiti na utumbo mkubwa.

Kutokana na changamoto hiyo Novemba 2019 Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa,alizindua Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza ambayo hufanyika wiki ya pili ya Novemba kila mwaka ili watu wafahamu magonjwa hayo ni kitu gani na kuchukua hatua.

Mwandishi wa makala hii Baltazar Mashaka,kabla ya kufanyika maadhimisho ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yanayofanyika mkoani Mwanza kitaifa mwaka huu,alifanya mahojiano na Mtaalamu wa Afya na Mazoezi wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) Dk. Waziri Ndonde,ambaye alizungumzia umuhimu wa kufanya mazoezi.

Anasema ili kujenga jamii isiyo na magonjwa yasiyoambukiza,wanaendelea kutoa elimu kwa watu wa makundi mbalimbali wakiwemo waandshi wa habari ili wasaidie kuelimisha jamii na wananchi wasiendelee kukumbwa na maradhi hayo.

Dk. Ndonde anasema elimu inayotolewa kwa waandishi wa habari inalenga kujenga uelewa wa kujikinga wao wenyewe,pia watoe taarifa sahihi za magonjwa yasiyoambukiza ili kujenga uelewa mpana kwa jamii na wajikite kuandika habari za kuelimisha jamii kuhusu magonjwa hayo wapate kufahamu athari zake.

Anasema magonjwa yasiyoambukiza yanasababishwana mambo matatu, moja kukosa usingizi wa kutosha,pili kutoshughulisha mwili (kufanya mazoezi) na kula vyakula bila mpangilio unaotokana na aina au makundi matano ya vyakula.

“Elimu hiyo ikiwafikia kwa usahihi na upana itawawezesha Watanzania kujenga tabia ya kufanya mazoezi angalau dakika 30 kwa siku ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanayochangiwa na kutokushughulisha mwili,”anasema Dk. Ndonde.

Kwamba zipo sababu nyingi zinazochangia magonjwa hayo na jinsi mfumo wa afya ulivyo na ili binadamu awe na afya bora anahitaji kula vizuri,kufanya mazoezi na kupata usingizi si chini ya saa 7 kwa mtu mzima.

Kwa mujibu wa Dk.Ndonde hayo matatu yakizingatiwa yatamwepusha mtu kupata magonjwa yasiyoambukiza kwa sababu anapolala kinga na mwili unajengeka baada ya kufanya shughuli za kila siku.

“Kushughulisha mwili kwa ajili ya afya kunauwezesha kufanya kazi,kutembea ama kuendesha baiskeli na kushiriki michezo na buradani.Tunakula na kupumua ili kuupa mwili nguvu ya kufanya hivyo,”anasema.

Mtaalamu huyo wa Afya na Mazoezi anasema tunapozaliwa misuli yetu haijui kazi kutokana na kulala tumboni mwa mama miezi tisa bila kujishughlisha,miezi sita baadaye tuanaanza kuketi ambapo zaidi ya mwaka mzima tunahitaji kujifunza kutembea na kukimbia.

Anasistiza kuwa uzoefu huo ni kwa sehemu zote mwili yakiwemo mapafu na moyo na tunahitaji kuendelea kutumia misuli yetu karibu kila siku ili kudumisha uzoefu huo kwa sababu bila kujishughulisha misuli inasahaujisni ya kutumia sukari na kutojishughulisha ni moja ya visababishi vya kisukari,saratani,magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Dk. Ndonde anasema Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa kutoshughulisha mwili kunachangia asilimia 6 ya vifo vyote duniani,asilimia 17 ya magonjwa ya moyo na kisukari,asilimia 12 kuanguka kwa wazee na aslimia 10 ya saratani za matiti na utumbo mkubwa.

“Binadamu anapofanya kazi au kushughulisha tishu za mwili wake zinaharibika,muda wa kulala una uwezesha mwili kujitengeneza (kujijenga),pia moyo kama ulikuwa na hitlafu utajikarabati wenyewe na mtu asipopata muda wa kulala ni rahisi kupata msongo wa mawazo,”anasema.

Mtalaamu huyo wa Mazoezi na Afya anaeleza kuwa mtu anapokosa muda wa kulala vizuri kuna uwezekano wa moja kwa moja wa kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, pia watoto wasipoata usingizi ukuaji wao unakuwa si mzuri.

Takwimu za dunia mwaka jana zinaonyesha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu yalisababisha vifo vya watu milioni 18 sababu kubwa ikiwa ni kutopata usingizi wa kutosha,pia takwimu za 2012 za WHO na Wizara ya Afya nchini, asilimia 33 ya vifo vilitokana na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Dk.Ndonde anashauri njia ya kuepuka wazingatie aina ya ulaji wa vyakula vya asili,wapunguze matumizi ya pombe,uvutaji wa tumbaku na vitu vinavyotajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa magonjwa yasiyoambukiza,hayana vimelea vinavyoweza kusambazwa isipokuwa yanatokana na uzembe wa mtu au kurithi.

Anasema zipo njia kuu tano za kushughulisha mwili:kazini (shuleni,nyumbani na ofisini),usafiri tunaotumia,kushiriki michezo mbalimbali,burudani na kazi za kijamii na tendo lolote linalohusisha misuli huongeza mapigo ya moyo au kasi ya kupumua au mwili kutoa jasho,liwe ni kazi, kusafiri,michezo au burudani.

Hivyo mtu asipofanya mazoezi,anakula mara tatu kwa siku ni hatari kwa afya yake kwa sababu haviwezi kutumika kikamilifu na badala yake hurundikana mwilini na kuwa chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu,matatizo ya moyo,kisukari,saratani na uzito uliopitiliza.

Kundi jingine lililo katika hatari lisipopata usingizi wa kutosha ni wana michezo,majeraha yao hayawezi kupona,pia watu baiskeli na wanaofanya kazi nguvu majeraha ya mwili hayaponi kwa sababu wanapotembea sana na kuendesha baiskeli mwili unajeruhiwa.

“Muda wa kulala majeraha yanajikarabati yenyewe ndiyo maaana tunasistiza watu wazingatiye na kutimiza mambo matatu ya kula mlo kamili,walale si ya saa 7 na wafanye mazoezi kwa muda usiopungua dakika 30 kwa siku.

Mtaalamu huyo anasema mazoezi hufanya mwili kutumia chakula cha ziada mwilini, yanaufanya kuwa mkakakamavu na kuepuka magonjwa yasiyoambukiza,kwa sababu magonjwa hayo yanaongezeka kwa kadri miaka inavyokwenda ni muhimu Watanzania wakatumia mbinu za kitaalamu kukabiliana nayo.

Anabainisha kuwa ni vizuri kula milo mitatu iliyo kamili zikiwemo mboga za majani na matunda,tuepuke kutumia sukari na chumvi nyingi kupita kiasi,chakula kiliwe saa mbili kabla ya kulala na si vizuri kulala baada ya kumaliza kula,unaposubiri kulala jishughulishe.

Anatahadharisha kuwa wafanyakazi wa maofisini na walioajiriwa serikalini kuwa,wapo hatarini kuugua magonjwa yasiyoambukiza kwa sababu hutumia muda mrefu kufanya kazi zao wakiwa wamekaa.

Anaonya kuwa wafanyakazi wa serikali wapo hatarini kuugua magonjwa yasiyoambukiza kutokana na kutumia muda mrefu kufanya kazi ofisini,pia wana kwenda na kutoka ofisini kwa kutumia magari.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya watu wasiofanya mazoezi mara kwa mara wanakuwa hatarini kuugua magonjwa yasiyoambukiza,pia mazoezi hufanya mwili kutumia chakula cha ziada mwilini na kuufanya mkakakamavu na kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.

Aidha kufanya mazoezi kuna faida nyingi kama kubaki kijana muda mrefu,kudhibiti unene,sukari na mafuta yaliyozidi mwilini na kuepuka kujenga shinikizo la damu,kisukari,ugonjwa wa moyo na saratani.

Pia kunajenga misuli ambayo husaidia kutumia nishati ya ziada na hivyo kuepuka unene,kujenga mifupa na ukuvunjuvu wa viungo, kupunguza msongo wa mawazo na uchovu, kuongeza kinga ya mwili,kuimarisha hisia na kuongeza ufanisi wa akili.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima anasema Kauli mbiu ya Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza yanayofanyika Kitaifa mkoani humu mwaka huu ‘Badili mtindo wa Maisha,Boresha Afya’ inalenga kuwahamasisha Watanzania kuachana na tabia bwete pamoja na mitindo ya maisha inaayosababisha waugue magonjwa yasiyoambukiza.

Anasema miongoni mwa tabia hizo ni kutofanya mazoezi,kula vyakula vyenye wingi wa mafuta,sukari na chumvi,matumizi ya tumbaku, dawa za kulevya na unywaji wa pombe uliokithiri.

Malima anasema takwimu zinaonyesha kuwapo ongezeko la magonjwa hayo kutoka watu milioni 4 mwaka 2018 hadi kufikia wagonjwa milioni 4.8 mwaka 2022 na kusababisha ongezeko la gharama za matibabu jambo hatari katika mfumo wa maisha na kiuchumi.

Anaonya kuwa ongezeko hilo linaathiri maisha,afya,jamii na uchumi na kuleta madhara hatimaye kusababisha vifo vya mapema lakini pia yanaigharimu serikali fedha nyingi za kuwahudumia wenye chagamoto hiyo.

“Magonjwa haya siyo tishio tu ulimwenguni bali hata hapa nchini,katika miaka 60 iliyopita magonjwa haya yalikuwa yanasababisha asilimia 20 ya vifo, kwa sasa yanachangia zaidi ya asilimia 34 hadi 40 kwa baadhi ya mikoa,” anasema Malima.


Changamoto hiyo ilisababisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Novemba 2019 kuzindua Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza ambapo maadhimisho ahufanyika wiki ya pili ya Novemba kila mwaka ili watu wafahamu magonjwa hayo ni kitu gani.


“Kipekee nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa chanzo cha hamasa ya watu kufanya mazoezi tangu akiwa Makamu wa Rais,anayapa msukumo wa kipekee, kila Mmoja wetu awekeze zaidi katika huduma kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na kuchukua tahadharizaidi ashiriki maadhimisho ya mwaka huu,”anashauri.

Share To:

Post A Comment: