Na Birigitha Kimario/SERENGETI


Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limefungua geti jipya maarufu kama Handajenga katika Hifadhi ya Taifa Serengeti wilayani Bariadi mkoani Sumiyu. 

Uzinduzi wa geti hilo lililopo magharibi mwa Hifadhi umefanyika jana ikiwa ni siku ya kwanza ya wiki ya maandalizi ya mbio maarufu kama “Serengeti Safari Marathon” ambayo inatarajiwa kufanyika Novemba 12, 2022 Serengeti.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa geti hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Lupakisyo Kapange, alisema

“Uwekezaji uliofanyika hapa katika wilaya yetu ya Bariadi ni fursa ya kufungua uchumi katika maeneo haya ambapo wananchi hawa walikuwa na kiu ya jambo hili na sasa kila mwananchi anatambua manufaa yatokanayo na shughuli za uhifadhi na utalii kwani kuanzia sasa watalii watakuwa wakipita hapa kupata huduma mbalimbali katika maeneo yetu.”

Aidha Mhe. Kapange aliwaasa wananchi kuzilinda na kuhifadhi Maliasili zetu kwa faida ya sasa na ya baadae na kuwaasa wananchi kubadilika na kuwa walinzi wa maeneo hayo yanayopakana na Hifadhi badala ya kuwa chanzo cha uharibifu wa maeneo hayo.

Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi -Serengeti, Izumbe Msindai, alisema kuwa lango hilo litakuwa chachu kwa wanabariadi kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa kuwa ni karibu kwa wananchi wa maeneo haya kutembelea Serengeti kupitia lango hili.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mbio “Serengeti Safari Marathon” - Mdinka Timothy, alisema kupitia mashindano ya mbio za mwaka huu 2022 zinazotarajiwa kufanyika Novemba 12, kwa ushirikiano na TANAPA wamekuja na nia ya kupanua wigo wa utalii kwa kuhamasisha utalii wa ndani hususani upande huu wa magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Geti la Handajenga ni fursa nyingine kwa TANAPA kutimiza adhma ya serikali ya kufikisha watalii millioni tano na mapato dola billioni sita ifikapo 2025, hivyo kufunguliwa kwa geti hili kutaongeza idadi ya watalii kutokea mikoa ya Mwanza na Simiyu kutembelea Hifadhi y’a Taifa Serengeti ambayo kwa mara nne mfululizo imeibuka kidedea kwa kuwa Hifadhi Bora Afrika.

Ufunguzi wa geti la Handajenga umeenda sambamba na mashindano ya mbio za baiskeli ambapo wanawake waliendesha kilometa 40 na wanaume waliendesha baiskeli kilometa 80
Share To:

Post A Comment: