Hali si shwari ndani ya chama cha waendesha bodaboda Jiji la Arusha (Uboja) baada ya kubainika zaidi ya Shilingi 400 milioni zimetolewa kwenye akaunti ya chama hicho huku baadhi ya fedha hizo zikidaiwa kutumika kisiasa.

Fedha hizo zinadaiwa kutolewa kwenye akaunti ya umoja huo kuanzia mwaka 2018 hadi 2021 katika mazingira ya kutatanisha na baadhi ya waliokuwa viongozi kwa kishirikiana na watu wengine bila wanachama kupewa taarifa yeyote

Katibu wa Umoja huo, Hakimu Msemo akizungumza na Waandishi alidai fedha hizo zilikuwa ni msaada kutoka kwa wahisani pamoja na michango ya marejesho ya wanachama wa chama hicho katika kipindi hicho.

Msemo alisema fedha hizo zimetolewa kwenye akaunt ya chama hicho kuanzia 2018 bila utaratibu na hivyo wameomba Serikali iwasaidie kupata haki yao kwani kwa zaidi ya miezi mitatu sasa wameshinda kujua hatma yao.

Kwa mujibu wa Msemo, alisema endapo fedha hizo zikirudishwa katika akaunti yao zitawasaidia kuendelea kukopeshana pikipiki kwa wanachama wao zaidi ya 12,000 waliopo katika Kata 25 za Jiji hilo la Arusha katika mkoa wa Arusha.

"Tunashukuru Benki ya NMB wametupa taarifa zote za kutolewa kwa fedha tangu kufunguliwa akaunti ambapo tumebaini fedha kutolewa kwenye matawi mbalimbali bila kufuata taratibu," alisema katibu huyo wa Uboja.

Alidai wamebaini kiasi cha Shilingi 120 milioni kilitolewa April 6, 2018 kupitia tawi la NMB Ngarenaro kwenda akaunti ya moja ya Jumuiya za chama kimoja cha siasa na wameonana na viongozi wao na wamekiri kupatiwa fedha hizo.

Kiongozi mmoja wa Jumuiya hiyo alikiri kupokelewa fedha katika jumuiya hiyo na kueleza fedha hizo zilitumika kwa ajili ya kuwakopesha wanawake ili kujikwamua na umasikini kama ilivyokuwa kwa bodaboda hao walivyokopeshwa pikipiki.

"Hizi fedha kama unakumbuka zilikuwa zinakusanywa na Mbunge Mrisho Gambo na wafadhili wengine sisi tulipewa ili kuwakopesha wanawake wa Jiji la Arusha,” alisema kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini. 

Mwenyekiti umoja wa bodaboda jiji la Arusha, Okelo Constantine aliiomba serikali kutoa maelekezo kwa vyombo vya dola kulishughulikia suala hilo kwa uharaka zaidi ili kuwakwamua wanachama wao wanaosubiri mgao wa pikipiki.

Alidai wanachama hao 12,000 huchangia mapato ya serikali kwa kukata leseni ya udereva Sh70, 000 kila mmoja kwa miaka mitano, Latra 17,000 Kila mwaka na mafuta ya Sh5, 000 kwa siku huwawezesha kuchangia mapato mengi kwa Taifa.

Kwa upande wake, Msemaji wa chama hicho, Joshua Samwel alidai wapo wadau wanaotaka kuwasaidia bodaboda 100 kwa kuanzia kulipa Sh100 milioni  lakini wanakosa fedha za kuanzia kwani akaunti yao ina Sh2 milioni tu.

Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda alikiri kupokea malalamiko ya viongozi na wanachama wa chama hicho na kusema,"uchunguzi wa malalamiko haya unafanyiwa kazi na vyombo husika vya dola wawe na subira.”

Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo ambaye alikuwa mmoja wa wasimamizi wa fedha hizo, akizungumza na wanachama wa Uboja wiki iliyopita, alishauri waliokuwa viongozi wa umoja huo watafutwe ili warejeshe fedha hizo.

Share To:

Post A Comment: