Mratibu wa zao la Pamba nchini kutoka Kituo cha Utafiti cha Kilimo Ukiliguru Dk. Paul Saidia (wa kwanza kushoto) akifuatilia tukio la utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi wa 'Beyond Cotton' unaolenga kuinua thamani ya zao la pamba kwenye mnyororo wa thamani kwa wilaya za Kwimba, Magu na Misungwi jijini Mwanza-unaofadhiliwa na Brazil kwa kushirikiana na Tanzania kwa gharama ya Dola 930,118 (Tsh.Bilioni 2.17) na kutekelezwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) na Bodi ya Pamba (TCB). Wengine pichani ni wataalamu mbalimbali watakaoungana na taasisi hizo kutekeleza mradi huo.

.Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), David Basley akikagua na kufanya uhakiki wa vifaa mbalimbali vitakavyotumika kufundishia wakulima wa pamba kupitia mradi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum kali aliyevaa suti (katikati) akiwa na wataalamu mbalimbali wanaotekeleza mradi wa kuongeza thamani kwenye zao la pamba ndani ya wilaya hiyo

Mkufunzi Mwandamizi wa masuala Lishe kutoka Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Campina Grande nchini Brazil, Profesa Vannile Penoa, akitoa mafunzo ya lishe bora kupitia mradi huo kwa wakulima wa pamba wilayani Magu.

Mtaalamu wa zao la pamba kutoka WFP, Joelcio Carvalho akiwaelekeza wakulima namna ya kutumia teknolojia ya kupanda mbegu mbalimbali kwa kutumia mashine maalumu.

Mmoja wa wakulima akiwa kwenye mazoezi kwa vitendo ya namna ya kutumia teknolojia ya mashine rahisi ya kupandia (planter) mbegu za pamba na mazao mengine bila ya kuinama.
Mtaalamu Mwandamizi wa masuala ya lishe na virutubishi kutoka TARI Ukiligulu Dk. Calesma Chuwa (wa kwanza kulia) akisimamia utekelezaji wa mafunzo kupitia mradi wa 'Beyond Cotton' kwenye eneo la kuboresha lishe kwa wakulima.

Mmoja wa wataalamu wa mradi huo, Profesa Luderlandio Andrade aliyevaa miwani shimoni akiwaelekeza mafundi na baadhi ya wakulima namna ya kujenga tenki kwa ajili ya teknolojia ya kuvuna maji ya mvua yatakayosaidia kuendesha kilimo cha mbogamboga na matunda hata wakati wa msimu wa kiangazi lakini pia kama kituo cha kujifunzia teknolojia hiyo kwenye eneo la lishe na namna ya kujiongezea kipato.Mratibu wa Lishe kutoka Wizara ya Kilimo Magreth Matai akitoa mafunzo kwa akinama wa wilaya ya Magu kupitia mradi huo.

 Wataalamu wa mradi huo wakitoa mafunzo ya namna bora ya kupima hali ya hewa kwa kutumia kifaa maalumu cha kupima kiasi cha mvua kabla ya kupanda pamba maarufu 'rain gauge'

Mratibu wa zao la Pamba nchini kutoka Kituo cha Utafiti cha Kilimo Ukiliguru ambaye pia ni mkurugenzi wa kituo hicho Dk. Paul Saidia (aliyesimama) akizungumza na wataalamu mbalimbali wa mradi huo muda mfupi kabla ya kuanza utekelezaji wake kwenye wilaya za Magu, Kwimba na Misungwi mkoani Mwanza.

Mtaalam kutoka Bodi ya Pamba Nchini (TCB) Renatus Luneja akitambulisha wageni mbalimbali wanaotekeleza mradi huo ndani ya Wilaya ya Magu. Bodi hiyo ni miongoni mwa taasisi zinazotekeleza mradi wa Beyond Cotton. 

Na Godwin Myovela, Mwanza 

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) kupitia kituo chake mahiri cha Ukiliguru kimehamasisha wananchi kutumia fursa ya msimu huu wa kilimo kuzalisha zao la pamba kwa tija, ubora na kwa kuzingatia agronomia stahiki ili kupata matokeo tarajiwa kwa manufaa chanya ya ukuaji uchumi kwenye mnyororo wake wa thamani.

Kwa mujibu wa Tari Ukiliguru, zao hilo la kimkakati ambalo linaongoza kwa kuwa na faida kubwa za kiuchumi ikilinganishwa na mazao mengine, linatajwa kama kiini cha malighafi muhimu kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo, nguo, pamba za hospitali, magodoro, mazulia na mito ya viti.

Mratibu wa zao la pamba nchini Dk. Paul Saidia alitoa hamasa hiyo wakati akishiriki utekelezaji wa mradi wa 'Beyond Cotton' unaofadhiliwa na Brazil kwa kushirikiana na Tanzania chini ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na Bodi ya Pamba (TCB) unaolenga kuinua tija ya zao la pamba kwa wilaya za Magu, Kwimba na Misungwi mkoani hapa.

Saidia ambaye pia ni Mkurugenzi wa kituo cha Tari Ukiliguru alisema hata mbegu za pamba ambazo hazitumiki kwa kupandwa na wakulima bado zina faida; kwani hutumika kwa kusagwa katika viwanda kwa ajili ya kutengeneza mafuta ya kula, margarine na sabuni-huku mashudu yake yakitumika  kama chakula cha mifugo na mboji.

Aidha, alifafanua kwamba kama mkulima atajifunga mkanda na kuzalisha robota moja ya pamba yenye kilogramu 227 ni dhahiri baada ya uchakataji itakwenda kuzalisha suruali za 'jeans' 215, mashati 750, fulana1200, soksi 4300 na kaptula 2100.

Zaidi kwa robota moja hiyo hiyo mtaalamu huyo alisema mkulima atazalisha idadi ya shuka za kitanda za futi 3 zipatazo 250, nepi 3000 na pamba za kuondolea uchafu masikioni kwa idadi ya 680,000 sambamba na mti wake kuchakatwa na kutumika kama mkaa mbadala.

"Ninajaribu kuainisha tija ya kilimo cha pamba na matokeo yake kwenye mnyororo wa thamani na upana huu wa soko ndani na nje ili kila mtanzania aone fursa zilizopo na azichangamkie," alisema Saidia.

Hata hivyo, katika muktadha wa mzunguko wake wa kibiashara alisema Tani moja pekee ya mbegu ina uwezo wa kuzalisha mpaka lita 200 za mafuta ya kula, kilo 500 za mashudu, kilo 300 za pumba na takribani lita 40 za magwanji ambayo hutumika kama malighafi ya kutengenezea sabuni.

Alisema kwa sasa ni mikoa 17 tu nchini inayolima pamba ambayo imeendelea kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa dunia ambapo kila mwaka linakadiriwa kuingiza takribani Dola Milioni 120 (Bilioni 27.6)

"Pamoja na kwamba ni mikoa hii michache inalima bado mchango wake ni mkubwa, sasa kama tutahamasishana na watanzania wakahamasika nadhani hapa tutachangia vizuri ajenda yetu ya 10/30," alisema Saidia na kusisitiza;

Pia kilimo hiki ni mwafaka wa falsafa ya waziri wa sasa wa kilimo, Hussein Bashe ambaye anaamini katika dhana ya 'kilimo cha kibiashara'  kwa maana ya kuuza bidhaa za kilimo zilizochakatwa kwa matokeo chanya kwenye kukuza uchumi, ongezeko la tija na fedha za kigeni kama mkakati wa ajenda 10/30 ifikapo 20/30.  

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: