Na. Immanuel Msumba; Longido

Katika kituo cha Afya Longido, nakutana na Bi Maiyasa Olekumbe, Mkazi wa Kijiji cha Engikaret. Katika mazungumzo yetu, anaeleza kuwa kutoka katika kijiji anachoishi hadi kituoni hapo ni zaidi ya kilomita 40. Asubuhi hii ametumia nauli shilingi Elfu ishirini (20,000) kwa usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda.

Taarifa yake inanipa mawazo kidogo. Natambua tuna changamoto na mafanikio makubwa katika sekta ya Afya. Je? Takwimu hizo haziakisi hali halisi?

Nchini Tanzania serikali kwa kushirikiana na wadau imepiga hatua katika kuboresha sekta ya afya hususan huduma za wajawazito na watoto chini ya miaka 5 zinazolenga kuokoa maishaya mama na mtoto. 

Tovuti ya Tanzania https://www.tanzania.go.tz/directories/hospitals inaonesha Tanzania kuwa na hospitali za Rufaa sita, za mikoa ishirini, za wilaya themanini na tano na zahanati 702.



Tovuti ya Serikali ikionesha idadi ya hospitali nchini Tanzana. 

Licha ya mafanikio hayo lukuki bado kuna changamoto mbali mbali ikiwemo;

 Ongezeko la Watu.

Ripoti ya sensa yam waka 2022, inaonesha Idadi ya watu Tanzania Bara imeongezeka kutoka watu 43,625,354 mwaka 2012 hadi watu 59,851,347 mwaka 2022. Hivyo, japokuwa kuna ongezeko la hospitali na Zahanati, idadi kubwa ya watu inafanya mzigo wa utoaji huduma za afya kuwa mzito zaidi.

Matokeo ya Sensa 2022


Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

Pamoja na jitihada za Serikali za kuhakikisha kwamba, dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vinapatikana, bado kuna upungufu na matatizo ya upatikanaji wake katika vituo vya kutolea huduma za afya na hivyo kuathiri utoaji wa huduma bora.

Maiyasa Olekumbe ni Mkazi wa Kijiji cha Engikaret Katika Kata ya Engikaret Tarafa ya Longido  anaeleza kuwa kutoka katika kijiji anachoishi ni zaidi ya kilomita 40 hadi kufika katika kituo cha Afya, huku akitakiwa kulipa nauli shilingi Elfu ishirini (20,000) kwa usafiri wa bodaboda.

Kituo cha Afya Longido


Tangu saa tatu asubuhi yupo kwenye foleni na mgonjwa wake kwa ajili ya kungoja kupata matibabu, kinachomshangaza amekaa kwenye foleni kwa zaidi ya masaa matano lakini kwa sasa mgonjwa wake ambaye ni mkwe wake ameingia katika chumba cha Daktari anaendelea kupatiwa matibabu tulivyokuwa tunatoka nyumbani alikuwa anatueleza kuwa kichwa kinamuuma sana na kifua kinabana kwa mbali.

"Nimenunua dawa za shilingi elfu mbili na mia tano na sindano za elfu kumi na moja lakini bado na ambiwa kwa sasa nahitaji dawa ya shilingi elfu arobaini, daktari anasema nimpe hela maana dawa nyingine zipo hapa hospitalini na nyingine ataenda kununua yeye aje achanganye kwenye trip".

Bi Maiyasa Olekumbe akiwa nje ya kituo cha Afya Longido.


"Tokea nimekuja napewa tu hizi risiti za mkono lakini sipewi karatasi yoyote ya kuonesha mgonjwa wangu anaumwa nini na amepimwa nini napewa hizi karatasi zenye nembo ya halmashauri na kuandikiwa mara elfu tano, mara elfu kumi na moja". Alisema

Maiyasa hayuko peke yake. Namnyaki Sendeu ambaye ni mkazi wa Kata ya Longido Mjini amedai kuwa kwa muda mrefu kumekuwepo na upungufu wa wahudumu katika Kituo cha Afya Longido huku miundombinu yake ikiwa ya zamani hali inayo sababisha wagonjwa kuchelewa kupata huduma za afya, hali inayohatarisha maisha ya wagonjwa na wajawazito.

Anasema wakazi wengi wilayani hapa wanaotegemea kupata huduma za afya katika Kituo cha Afya nao hali ile inawakatisha tamaa kama yeye. Kwani hata wananchi waliojiunga katika mpango wa huduma ya Afya ya Jamii hawapati huduma kama inavyohitajika.

"Nikienda Kituo cha Afya pale sipati huduma kabisa kwa sababu wanataka hela nalazimika kwenda mpakani mwa nchi yetu Namanga ama Arusha kwenye Zahanati ya mtu binafsi maaana nikienda kule natoa elfu 30 wala sitoi hela nyingi napatiwa matibabu na dawa wala siongezi hela yoyote".

"Wakati wa mama kwenda kujifungua kama Mungu akikusimamia ukijifungua salama utalipa laki na nusu ila kama utajifungua kwa upasuaji utalazimika kulipia laki moja na themanini hapo bado hujaweka dawa na huduma nyingine za vitanda na matibabu". Aliongezea


Uelewa wa Wananchi.

Kama hiyo haitoshi, kuna changamoto nyingine kubwa ambayo inatumiwa na watoa huduma za afya kwa manufaa yao. Namnyaki anasema “sisi kama jamii ya kimasai hatujui kusoma hivyo ukienda kupatiwa matibabu unaandikiwa karatasi ya dawa ina maelezo mengi unaambiwa ni ya dawa tunatoa hela tunanunua na nyingine tunaenda kununua nje ya Kituo cha Afya”

Maelezo yake yanashabihiana na takwimu rasmi. Kwa mujibu wa UNESCO, kiwango cha sasa cha wanaojua kusoma na kuandika nchini Tanzania ni asilimia 77.89. Wengi wasiojua kusoma ni kutoka jamii kama za Kimasai.

Lakini je, nini kifanyike? Namnyako anaeleza “Nimejaribu kuwashirikisha Mwenyekiti wetu wa Kijiji na Diwani kuhusiana na swala la huduma za Afya ambazo tunazipata pale Kituo cha Afya lakini hawatusaidii kabisa kwa msaada wowote hata wa kifedha”.

Niiombe serikali kuangalia namna gani bora kwa sisi wamama wa jamii ya kimasai tuweze kupatiwa huduma wakati wowote wa kujifungua hata kama hatuna fedha tuweze kusaidika na sio kuchagua huyu hana fedha huyu hana wote tupatiwe huduma kwa usawa.Upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya.

Aidha, upatikanaji wake ni moja ya vivutio kwa wananchi kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya. 



Share To:

Post A Comment: