Na Immanuel Msumba ; Monduli

Mfumo wa Elimu na mafunzo wa sasa hauliwezeshi Taifa kukidhi ongezeko la mahitaji ya rasilimaliwatu kulingana na vipaumbele vya Taifa kwa sababu takwimu za mwaka 2000 hadi 2012 zinaonyesha kuwa ni wastani wa asilimia 5 tu ya wahitimu wa darasa la saba ndiyo wanaofaulu na kuendelea hadi kufikia elimu ya sekondari ya juu na  asilimia 4.3 hujiunga na mafunzo ya ufundi stadi, asilimia 1.2 hujiunga na elimu ya ufundi wastani wa asilimia 4  ya wanafunzi hao ndiyo wanaofaulu na kuendelea hadi kufikia elimu ya juu.

 Kwa mwenendo huo, ni dhahiri kwamba Taifa litaendelea kuwa na nakisi ya wataalamu, kama hatua madhubuti za kuongeza fursa na kuinua ubora wa elimu hazitachukuliwa kwa sababu lengo la serikali  ni kuwa na rasilimaliwatu mahiri na ya kutosha ili kukidhi mahitaji ya sekta mbalimbali kwa maendeleo ya Taifa. 

Aidha wakati serikali ikiendelea kuweka mazingira rafiki ya kuhakikisha lengo hilo linafikiwa hali ni tofauti katika Wilaya ya Monduli ambapo licha ya uwepo wa rasimali watu (waalimu) wa kufundisha wanafunzi wanalazimika kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kutokana na ukame uliokithiri kwa baadhi ya maeneo wilayani humo hali inayosababishwa lengo la serikali kutokufikiwa.

September 30 mwaka huu nilitembelea  shule ya sekondari Nanja iliyopo katika Kijiji cha Mti Mmoja na kukuta idadi kubwa ya wanafunzi  hawapo shuleni na nilipotaka kujua ni kwanini nilijulishwa kwamba wamekwenda kutafuta maji Kijiji cha jirani  kwa ajili ya kuoga na kufua zao sare za shule.

Kufuatia hali hiyo nililazimika  kwenda kuona sehemu ambayo wanafunzi hao wanachota maji kwenye bwawa  la kunywesha mifugo maji ambalo limejaa matope hali inayowalazimu wanafunzi hao kwenda na vikopo vidogovidogo kwa ajili ya kuchota maji hayo.

"Nilitembea umbali wa zaidi ya Kilomita tatu kutoka shuleni hadi kukuta bwawa hilo lakini cha ajabu nilikuta maji yakiwa ni machafu yamejaa matope huku wanafunzi wakiendelea kufulia sare zao za shule yakiwemo mashati meupe".

Baada ya kuzungumza na wanafunzi hao ambao hawakutaka majina yao kuandikwa kwenye Blog hii wakihofia kuchapwa na waalimu wao au kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu  walidai kuwa wanakutana na chanagamoto mbalimbali pamoja na viashawishi kutoka kwa madereva wa pikipiki na vijana wa jamii ya Kimasai wanaotoka kuchunga mifugo wanapoileta kunywa maji.

Akizungumza kwa uchungu mmoja wa wanafunzi hao (jina linahifadhiwa)  anayesoma kidato cha kwanza shuleni hapo alidai kuwa  tangu amejiunga na shule hiyo anapata wakati mgumu  sana kwenye masomo yake kwani anatumia muda mwingi wa masomo kwenda kutafuta maji umbali wa kilomita zaidi ya tatu hali inayomsababishia kushuka kitaaluma.

"Tunaishi kwa shida sana hapa shuleni kwa sababu hakuna maji tunalazimika kwenda kuchota maji yaliyojaa tope kwenye mabwawa ya kunywesha  mifugo na baya zaidi maji ni machafu mno yamejaa tope wakati mwingine tunawashwa mwili mzima na kutokwa vipele kutokana na maji machafu tunayotumia kuogea na kufulia kwa sababu sare zetu za shule tukishazifua huwa hatupigi pasi"

"Kibaya zaidi wenzetu wa kidato cha nne huwa hawaji  kuchota maji wanasubiri usiku wa manane tukiwa tumelala wanakwenda jikoni kuiba maji ambayo yanaletwa hapa shuleni kwa ajili ya matumizi ya kupikia na kunywa hususani wenzetu wavulana hawana sana shida ya maji maana huwa hawaogi mara kwa mara wala kufua".

Mwanafunzi huyo amemuomba waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda kutembelea shule hiyo na kujionea adha kubwa wanayoipata ya ukosefu wa maji hali inayosababisha kukosa masomo kwa ajili ya kwenda kutafuta maji kwenye mabawa katika vijiji vya jirani.

"Hapa shuleni tuna umeme hivyo tunaiomba serikali ituchimbie kisima ili tuweze kupata maji ya uhakika badala ya kutumia muda mwingi kwenda kuteka maji tutumie muda huo kuhudhuria vipindi vya masomo".

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa kike wa kidato cha tatu  shuleni hapo amesema kutokana na hofu ya kubakwa au kufanyiwa vitendo vingine vya kikatili  pamoja na usumbufu wanaoupata kwa vijana wa kiume wa vijiji hivyo pamoja na baadhi ya waendesha pikipiki ameiomba serikali kuimarisha ulinzi wao kutokana na shule hiyo kutokuwa na uzio.

"Tukiwa njiani kwenda kutafuta maji tunakutana vishawishi vingi wakati mwingine baadhi ya waendesha pikipiki wanatutaka tuwe wapenzi wao ili watulee maji jirani na shule kiasha tukachukue lakini pia changamoto nyingine ni baadhi ya vijana wa vijiji hivi kututaka twe na mahusiano nao ya kimapenzi na tukiwakatilia wakati mwingine wanatukimbiza tukiwa tumebeba maji yanamwagika tunarudi shuleni bila maji,Tunaomba ulinzi ili tutuimize ndoto zetu za masomo".

"Mwanafunzi mwingine wa kidato cha pili anasema tangu afike shuleni hapo kumekuwa na ubaguzi mkubwa kwa wanafunzi kwa sababu wao wanatumia maji yanayoletwa na jeshi kwa ajili ya kuogea kufua pamoja na matumizi mengine ya nyumbani.Kwetu sisi tunaoana hii si sawa na ndiyo sababu shule haichimbiwi kisima kwa sababu waalimu hawana adha ya maji.Wangekuwa nayo ingekuwa wameshawasilisha changamoto kwa mamalaka husika na ingekuwa imeshatatuliwa"

"Mama yetu  Rais Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada za kumtua mama ndoo kichwani kwa kupeleka miradi ya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini na sisi wanafunzi wa Nanja sekondari ombi letu kwake tunaomuomba atusaidie sisi tupate maji hapa shuleni kwa sababu tuko hatarani kukatisha ndoto zetu za masomo ama kwa kubakwa au kufanyiwa vitendo vibaya vya ukatili".

 Diwani wa kata ya Lepruko Yonas Masiaya amesema shule hiyo iliyojengwa mwaka 2008/09 ina wanafunzi zaidi ya 600 ambao wanatoka katika Kata tatu za Sepeko,Lashaine na Lepruko ni kweli wanakabiliwa na  changamoto kubwa ya maji kwa sababu tangu kuanzishwa kwa shule hiyo hakuna juhudi zozozte za kupeleka maji ya uhakika  shuleni hapo.

"Tatizo kubwa la ukosefu wa maji  kwa wanafunzi wa shule hii sambamba na jamii inayozunguka eneo  hili ,wanafunzi wanazalimika kwenda kutafuta maji kwa zaidi ya kilomita tatu  kwenye bwawa la Nanja na maji hayo si salama kwa matumizi ya binadamu ni machafu sana hata ukiambiwa wanafunzi wanakwenda kuyatumia huwezi kuamini utawaonea huruma kwa jinsi yalivyo machafu hayafai kabisa"

'Diwani huyo anasema tuna mradi wa maji lendikiny'a ambao ulikuwa unagharimu zaidi ya milioni mia nane mkandarasi alishamaliza kazi yake lakini changamoto kubwa ni fedha kutoka serikali kuu ambazo hatujui zitakuja lini.Likini licha ya mradi huo alisema kuna maradi mwingine maji unaosimamiwa na Mamalaka ya Maji  Safi na uasafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) ambao unakwenda hadi Monduli lakini changamoto nyingine nifedha za kusambaza maji hayo kwenye kata mbalimbali ikwemo Sepeko.

"Kuna mradi wa Maji wa Hayati  Rais John Pombe  Magufuli alizindua Wilayani Arumeru eneo la Sambasha tunategemea huu mradi ukifika Monduli utaongeza nguvu na kupunguza kabisa tatizo la maji kwa sababu mradi huu ni mkubwa na ukifanikiwa utatatua changamoto kwa Vijiji kumi na tatu tunautegemea kwa kiasi kikuibwa"

Naye Mkuu wa Wilaya Monduli Frank Mwaisumbe amekiri kuwepo kwa changamoto ya maji shuleni hapo na siyo shule hiyo pekee kuna taasisi zisizopungua 24 zikiwemo za afya,elimu,sekta binafsi na nyingine za serikali ambazo hazina maji na kuna vijiji k17 ambavyo pia havina maji .

"Nikweli hii shule ya Nanja ipo katika Kijiji cha Mti Mmoja  na anakakabiliwa na changamoto kubwa ya maji lakini serikali tumeshabuni mradi wa vijiji 13 unaotoka kwenye mradi wa bilioni 520 kutoka Jiji la Arusha kwa hiyo katika mradi huo tutapata lita milioni tatu kwa siku na hivi sasa tunatafuta mkandarasi ili asaini mkataba ili ujenzi uanze mwaka huu na moja ya vijiji vitakavyonufaika ni Mti Mmoja ilipo sekondari ya Nanja".

Amesema wilaya inakabiliwa na uakame na mahitaji ya maji kwa siku ni lita milioni sita na mpaka sasa hivi tuna lita za ujazo milioni 2.5 ambazo zinapatikana kwa siku.Hata pale Monduli Mjini kuna baadhi ya Taasisi ambazo hazina maji na maji yanapatikana kwa zamu hivyo utaona ni jinsi gani tatizo lilivyo kubwa.Vijiji vinaendelea kutumia maji ya kwenye mabwawa ikiwemo Nanja sekondari lakini kwa bahati nzuri maji ya kunywa na kupikia wanapewa na jeshi kwa boza ambapo halsmahauri inaweka mafuta magari ya jeshi kwa jili ya kuwapelekea maji.
Share To:

Post A Comment: