Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora. 

Na Dotto Mwaibale, Singida 

WANANCHI wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, wamewataka Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Michael Matomora  kujiuzulu nyadhifa zao kufuatia kushindwa kusimamia vizuri mapato yanayokusanywa wilayani humo.

Hayo yamebainishwa na wananchi hao wakati wakizungumza na mwaandishi wetu kuhusu upotevu wa zaidi ya Shilingi Milioni 365 ambazo zinadaiwa kutafunwa na watumishi na mawakala waliozikusanya kama ushuru na kodi.

Wananchi hao wameeleza  kuwa Mwenda na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Michael Matomora wanatakiwa kuachia ngazi kwa sababu wao ndio watendaji wakuu wa wilaya hiyo lakini wameshindwa kusimamia mapato yanayokusanywa na kuishia kuliwa na watumishi wasio waaminifu na wakibaki wakilalamika licha ya vyombo vya dola kama TAKUKURU na Polisi kuwepo.

"Mwenda kinachomponza ni kuwa mpole na Matomora yeye akiwa mtendaji mkuu wa halmashauri hiyo kushindwa kuchukua hatua zozote huku akiangalia mapato yakipotea" alisema Samuel Makala mkazi wa Misigiri.

Mkazi wa Shelui, Elinipa Shango alisema viongozi hao wapepoteza sifa na hawana kasi anayoitaka  Rais  Samia Suluhu Hassan ya kukusanya mapato kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya ya Iramba, mkoa na Taifa kwa ujumla hivyo wanatakiwa kuachia ngazi.

Wananchi hao walisema kuwa mapema mwaka huu Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo aliagiza kurejeshwa kwa fedha hizo lakini licha ya kauli hiyo ya kiongozi mkubwa wa nchi hakuna hatua zozote zilichochukuliwa zaidi ya kuongezeka kwa kutafunwa fedha nyingine  hadi kufikia Sh.365 huku wafujaji wa fedha hizo wakiongezeka.

Walisema Watumishi na mawakala hao wanadaiwa kuzikusanya fedha hizo na badala ya kuzipeleka benki kwenye akaunti za serikali waliamua kuzitafuna na kuwa tabia hiyo imekuwa likijitokeza kila mwaka.

Kufuatia ubadhirifu huo Mkuu wa  Mkoa wa Singida,Peter Serukamba, ametoa siku saba kwa watumishi wa idara ya fedha wa halmashauri ya wilaya hiyo kuzirejesha Sh.milioni 365 ambazo zinadaiwa kutafunwa.

Serukamba alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wakuu wa idara, wahasibu na watendaji wa vijiji na kata na kueleza  halmashauri hiyo ndio inayoongoza mkoani hapa kwa watumishi wake kukusanya fedha na kuzitafuta bila kuzipeleka benki.

"Mumeenda kwenye masoko wananchi wema wamelipa ushuru na kodi lakini mtumishi tuliokupa jukumu la kukusanya fedha baada ya kuzikusanya badala ya kuzipeleka benki unaamua kuziweka mfukon maana yake tumekupa mtaji hili jambo haliwezekani," alisema.

Alisema katika kipindi chake akiwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kama kuna mtumishi anadhani hawezi kukusanya fedha za serikali na  kuzipeleka benki au halmashauri basi aache kazi hii haraka.

Serukamba alisema katika ufisadi huu kuna mambo mawili yanajitokeza inawekezekana kuna njama kati ya wakuu wa idara na wakusanyaji ambapo fedha hizo zikikusanywa wanagawana na hivyo serikali kukosa mapato.

Akizungumza katika mkutano huo Mkuu  wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, alisema tatizo hilo limekuwa sugu kwani mwaka jana watumishi na mawakala walikuwa wanadaiwa zaidi ya Sh.millioni 200 lakini mwaka huu deni limeongezeka na kufikia zaidi ya Sh.milioni 300.

Mwenda alisema wakuu wa serikali walishafika katika wilaya ya Iramba akiwamo Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa ambao waliagiza fedha hizo zilizotafunwa na watumishi zirejeshwe lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu.

"Jambo hili limekuwa la muda mrefu, mwaka jana watendaji walikuwa wanadaiwa zaidi ya Sh.milioni 200 pamoja na serikali kuchukua hatua kwa watumishi waliohusika cha kushangaza ufujaji umeongezeka na kufikia Sh.milioni 300 sasa," alisema.

Alisema wananchi ni haki yao kuhoji hasa pale wanapoona fedha za serikali zikifujwa kwani fedha hizo zaidi ya Sh.Milioni 360 ni nyingi na zingeweza kujenga hata kituo cha afya.

Alisema hatua walioichukua ni kuwafukuza kazi watumishi 17 waliohusika na ubadhirifu huo na Iramba kuwa ni halmashauri ya kwanza kwa kuwafukuza kazi watumishi wengi kwa wakati mmoja.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora alipopigiwa simu ili kupata  maoni yake kuhusu madai ya wananchi ya kuwataka wajiuzulu nyadhifa zao kwa kushindwa kudhibiti upotevu wa mapato simu yake iliita bila ya kupokelewa. 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: