Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigella ametoa wito kwa wachimbaji wadogo wa madini na wadau wote kushiriki katika Maonesho ya 5 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita.

Shigella ametoa wito huo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho hayo na kujionea huduma na bidhaa zinazotolewa katika Maonesho hayo.

"Naomba nitumie fursa hii kuwataka wachimbaji wadogo wa madini na wadau wote wa madini kushiriki kikamilifu katika Maonesho haya ili kupata elimu na mafunzo zaidi ya namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini," amesema Shigella.

Aidha, Shigella amesema Sekta ya Madini ni muhimu kwenye mchango wa uchumi wa Taifa ambapo amewataka wahusika kuendelea kuisimamia ipasavyo ili iongeze mchango wake kwenye Pato la Taifa.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watanzania kutumia mkaa wa mbadala wa mawe ambao ni rafiki kwa umazingira.

Dkt. Mwasse amesema STAMICO imekuja na teknolojia ya utengenezaji wa mkaa mbadala ambao unauzwa kwa bei nafuu na ni rafiki kwa mazingira.

Maonesho ya 5 ya Teknolojia ya Madini 2022 yanayoendelea mkoani Geita yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 03 Oktoba, 2022



Share To:

JUSLINE

Post A Comment: